In Summary

•Mchungaji Natasha aliombea masuala mbalimbali katika maisha ya msanii huyo  ikiwa ni pamoja na taaluma yake ya muziki.

• Bahati alifichua kuwa mhubiri huyo alimsihi arejee kwenye tasnia ya muziki wa injili ambayo aligura miaka kadhaa iliyopita.

Bahati akiombewa na mchungaji Lucy Natasha
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwimbaji wa zamani wa nyimbo za injili Kelvin Kioko almaarufu Bahati alikuwa na kipindi cha maombi na mhubiri maarufu wa Kenya Reverend Lucy Natasha wa kanisa la Empowerment Christian Church jijini Nairobi.

Katika kipindi hicho cha maombi ambacho Bahati alionyesha kwenye ukurasa wake wa Instagram, mchungaji Natasha aliombea masuala mbalimbali katika maisha ya msanii huyo  ikiwa ni pamoja na taaluma yake ya muziki.

Natasha alisikika akimwomba Mungu amwezeshe mwimbaji huyo kugusa maisha ya wengi kupitia muziki wa injili kama alivyokuwa akifanya kabla ya kugura tasnia hiyo.

“Baba mtumie kama sauti katika kizazi hiki, mtumie kama sauti katika kipindi hiki na kuwaongoza mamilioni ya watu kumjua Mungu wetu Yesu Kristo. Bwana Yesu natangaza athari yake haitaisha,” mchungaji Lucy Natasha alisikika akiomba.

Aliendelea kusali, “Ninaomba kwamba muziki wa injili ambao ataimba utagusa maisha, sio tu Afrika bali ulimwenguni. Mtumie kwa utukufu wako. Bwana nakushukuru kwa sababu Bahati ni sauti. Sauti ambayo utaitumia.."

Katika video iliyoshirikishwa na Bahati, mwanamke huyo wa Mungu alionekana akimshika mikono mwanamuziki huyo huku wakiwa wamekaa kwenye makochi akimuombea.

Katika taarifa yake, Bahati alifichua kuwa mhubiri huyo alimsihi arejee kwenye tasnia ya muziki wa injili ambayo aligura miaka kadhaa iliyopita.

“Pastor Rev Lucy Natasga anasema nirudi kwa gospel music.. Kwani nimekosea wapi?? #BornAgain,” aliandika Bahati.

Bahati alitangaza kugura injili mwaka wa 2020 lakini akaweka wazi kuwa imani yake kwa Mungu haikuwa imepunguka hata kidogo.

Mwanamuziki huyo alifichua hayo wakati wa mahojiano na mchekeshaji MC Jessy kwenye kipindi chake Jessy Junction.

“Injili ni Kristo. Nina Kristo moyoni mwangu na ninaamini katika Mungu na Mungu ndiye sababu ya mimi kuwa kileleni hivyo siwezi kumwacha Kristo,’’  alisema.

Alidai kwamba tasnia hiyo imeoza na kuweka wazi kuwa uamuzi wa kugura ndio bora zaidi ambao aliwahi kufanya.

“Nilipigwa vita sana katika tasnia ya injili lakini nilijua sifanyi muziki wa injili kwa ajili ya watu; Nilikuwa nikifanya kwa ajili ya Mungu.

Nimejitenga na tasnia ya injili kwa muda lakini si kutoka kwa Mungu. Kristo na Bwana ndiye mwokozi wangu binafsi,” alisema.

Mwaka wa 2021, alifichua kwamba alifunga siku kadhaa kabla ya kugura injili na kuanza kuimba nyimbo za mapenzi.

View Comments