In Summary

• Na kabla hawajapona donda hilo, Sapologuano Odeniumz tena amerudi na mjeledi ule ule kwenye video yao na kuiripoti pia.

Diamond na Jux
Image: Instagram

Wiki chache zilizopita tuliripoti kuhusu msanii wa kutokea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sapologuano Odeniumz ambaye amekuwa akivutana na Diamond na Jux kuhusu hakimiliki ya wimbo wa Enjoy.

Msanii huyo baada ya kuidungua audio ya kolabo hiyo, sasa tena amerudi kwa mara nyingine na safari hii ameiripoti video ya Enjoy ambayo vile vile imefutwa YouTube.

Audio ya wimbo huo ilipofutwa na YouTube baada ya Odeniyumz kuiripoti kuwa ilikuwa ni ngoma yake asili ambayo iliibwa na kufanyiwa uhariri wa kuboreshwa kiasi na Diamond na Jux ili kuzalisha wimbo wao wa Enjoy, msanii huyo alisema kwamba alichokuwa anakitaka ni mazungumzo kwa ajili ya kulipwa tu.

Lakini uongozi wa Jux na Diamond ulisita kufanya maongezi na yeye na baadae pia waliripotiwa kuangusha wimbo wake pia na baadae wakaja wakafanikiwa kuurudisha wimbo huo.

Lakini licha ya kufanikiwa kuirudisha audio YouTube, uongozi wa Jux ulisema wimbo huo haujawapa mapato yoyote kwani hauwezi tena ukatengeneza hela.

Na kabla hawajapona donda hilo, Sapologuano Odeniumz tena amerudi na mjeledi ule ule kwenye video yao na kuiripoti pia.

Video hiyo mpaka kudunguliwa ilikuwa imepata utazamaji wa Zaidi ya milioni ya tano lakini msanii huyo wa Kongo amesisitiza safari hii anachokitaja si hela bali ni kupewa hakimiliki zake.

“Ninachotaka ni hakimiliki tu, maana wao wananionesha dharau, kuna muda wanaongea vitu na baadae wanakuja kuvigeuka kwenye baadhi ya mahojiano ya vyombo vya habari,” alisema huku akisisitiza kwamba hatafuti kiki kwa kuwanyima Diamond na Jux usingizi.

Msanii huyo alisema kwamba hatokuja kukaa na kuona watu wakila kupitia jasho lake na ataendelea kumnyima Diamond usingizi hadi pale watakapokubali kuketi ili kuyamaliza.

“Kuhusu wao kuendelea kuingiziwa hasara, ni wao wenyewe waliyataka wenyewe maana tungeyamaliza kama hivi haya yote hayapo kwa sababu tulikuwa tunawaandikia lakini hawakutujibu hadi tukaamua kuchukua uamuzi wa kuripoti YouTube,” alisema.

Baada ya Diamond na Jux kusema kwamba sasa wanatathmini njia za kisheria dhidi ya Sapologuano msanii huyo pia alisema haogopi chochote kwani pia yuko tayari na vizuri kisheria.

“Hata sisi wenyewe tuko vizuri, wakija kisheria na sisi tutawapiga kisheria vile vile maana wasifikirie niko peke yangu, niko na menejimenti pia na wanasheria,” alisema kwa kutishia.

 

View Comments