In Summary

• Diamond alipakia pia video akiwa amewekewa mirija mingi kwenye mwili wake na akiwa amenyong’onyea kabisa kwenye kitanda kilichokuwa kimezungukwa na madaktari.

Diamond hospitalini
Image: Screengrb

Msanii Diamond Platnumz amewapa mashabiki wake taarifa mbaya ya kuugua kwake ghafla akiwa anajiandaa kwa shoo ya Wasafi Festival katika mji wa Arusha.

Platnumz kupitia Instagram yake alipakia video akiwa anahudumiwa katika kitanda cha hospitali na madaktari na kuandika kwamba alipatwa na homa wakati anajiandaa kuingia jukwaani kutumbuiza.

“Siku yangu ya leo ilianza vibaya sana Arusha, homa kali iliyopelekea hadi kulazwa kwa muda,” Diamond aliandika.

Aidha msanii huyo alifichua kwamba baada ya ganga ganga za waganga hospitalini, hatimaye aliweza kupata nafuu japo akawaomba mashabiki wake kuzidisha dua na maombi ili aweze kupata nguvu ya kutumbuiza kwenye tamasha hilo ambalo limekuwa likiendelea katika mikoa mbali mbali tangu mwezi Agosti.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa sasa naendelea vyema, naendelea kupata nguvu. Msiache kuniombea ili nipate nguvu Zaidi na kufanya vyema kwenye shoo ya WAasafi Festival,” aliwasihi mashabiki wake.

Hii si mara ya kwanza kwa nguli huyo aliyeleta mabadiliko makubwa kwenye muziki wa Bongo Fleva kulazwa.

Itakumbukwa mwishoni mwa mwaka jana, Diamond Platnumz alilazwa hospitalini baada ya kuugua ghafla jambo lililopelekea yeye kukosa kutumbuiza katika tamasha ambalo alikuwa ameratibiwa kutumbuiza la kufunga mwaka nchini Burundi.

Sawa na video ya sasa aliyopakia kwenye Instgram yake, Diamond alipakia pia video akiwa amewekewa mirija mingi kwenye mwili wake na akiwa amenyong’onyea kabisa kwenye kitanda kilichokuwa kimezungukwa na madaktari.

Mashabiki wake walifurika mitandaoni na kumtakia kheri njema na nafuu ya haraka huku wengine wakizusha kuwa huenda ni moja ya kiki zake za kila mara ambazo wamezoea kutoka kwake.

 

View Comments