In Summary

• "Inaweza kuonekana kama nilimuokoa Yoyo, lakini kwa kweli, Yoyo ananiokoa,” Nyong’o alimaliza.

• Mshindi huyo wa tuzo ya Oscar 2014 alisema kwamba paka wake mpya ambaye atakuwa rafiki wake wa karibu kipindi cha upweke anaitwa Yoyo.

Lupita Nyong'o
Image: Instagram

Wiki moja baada ya mwigizaji kutoka Mexico mwenye usuli wa Kenya, Lupita Nyong’o kuweka wazi kwamba penzi lake na Selema Masekela lilikuwa limekwisha, mrembo huyo sasa amepata faraja katika paka wa kuasili.

Nyong’o kupitia ukurasa wake wa Instagram wikendi iliyopita, aliweka wazi kwamba kwa muda mrefu hajawahi kuwa mpenzi wa wanyama wa kufugwa nyumbani lakini safari hii alielezewa umuhimu wa wanyama hao kumpa mtu faraja baada ya kuachwa.

Baada ya kuelezewa kwa ushawishi mkubwa, binti wa gavana wa Kisumu aliandamana sako kwa bako na rafiki huyo hadi katika boma la kufuga wanyama wa kuasiliwa na kumchagua paka aliyemfurahisha ambaye alisema kwamba atakuwa anampa faraja kipindi hiki anapojaribu kusahau yote yaliyotokea katika penzi lake na Masekela, Mmarekani mwenye asili ya Afrika Kusini.

Mshindi huyo wa tuzo ya Oscar 2014 alisema kwamba paka wake mpya ambaye atakuwa rafiki wake wa karibu kipindi cha upweke anaitwa Yoyo.

“Namtambulisha mwenzangu mpya, Yoyo!Kihistoria nimekuwa nikiogopa paka, lakini maisha yangu yalipobadilishwa mara moja hivi karibuni, sauti kidogo ilininong'oneza kwamba ilikuwa wakati wa kukumbatia mabadiliko na uwezekano mpya. Kwa hiyo, rafiki mpendwa (shurani sana Palmer Hefferan!) alinishika mkono kupitia mchakato huo na kunipeleka kutembelea makao yangu ya kwanza ya wanyama,” alisema.

Nyong’o alifichua kwamba kwa muda mrefu alikuwa anawaona kama wehu watu ambao walikuwa wamejaza picha za wanyama wa kuasili kwenye simu zao lakini baada ya kupigwa na upweke, aligundua maana na umuhimu wa kuwa na angalau kiumbe hai wa kukupa faraja.

“Nilimlea Yoyo kutoka Kituo cha Kuasili cha Marafiki Bora, na siku 3 ndani yake, nilijua singeweza kumchoka. Sikuwahi kuelewa watu ambao simu zao zilikuwa zimejaa picha na video za wanyama wao kipenzi - sasa mimi ni mmoja wa watu hao! Inaweza kuonekana kama nilimuokoa Yoyo, lakini kwa kweli, Yoyo ananiokoa,” Nyong’o alimaliza.

View Comments