In Summary

• Aliwahimiza wanaume kutafuta sifa zaidi ya kuvutia kando na zile za kimwili wanapofikiria kuoa.

• "Ikiwa unatafuta urembo basi utakata tamaa haraka. Ngoja nikushauri, unaweza kutafuta urembo lakini jiulize huyo mwanamke ana nini tena kando na urembo unaoupenda.

Christina Shusho
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki tajika wa nyimbo za Injili wa  Tanzania, Christina Shusho, ametoa ujumbe mzito akiwataka wanaume kufikiria upya mbinu zao za kuchagua wampenzi ambao wangetaka kuanzia nao familia.

Shusho alionya dhidi ya kutanguliza urembo katika kutafuta uhusiano wa kudumu.

Aliwahimiza wanaume kutafuta sifa zaidi za kuvutia kando na zile za kimwili wanapofikiria kuoa.

Shusho alisema kuwa urembo unaweza kubadilika kadri muda unavyokwenda kutokana na sababu mbalimbali hasa uzee. Pia alisema kuwa mapenzi yanaweza kupungua.

"Ikiwa unatafuta urembo basi utakata tamaa haraka. Ngoja nikushauri, unaweza kutafuta urembo lakini jiulize huyo mwanamke ana nini tena kando na urembo unaoupenda. Upendo utafifia. Nini kitakufanya bado uendelee kumpenda mke huyo ikiwa uzuri umetoweka na mapenzi kupungua?

Kijana yeyote anayetaka kuoa, zingatia jambo hilo. Kitu kipi ambacho bado kitakufanya uvutiwe na mwanamke huyo wakati urembo umetoweka na hata  baada ya mapenzi  kukosa nguvu tena,” Shusho alisema.

Shusho alisisitiza kuwa upendo lazima uwe zaidi ya mwonekano wa mwili, upendo wa hisia za kweli.

Mwimbaji huyo ambaye anatarajiwa kufanya tamasha la muziki nchini Kenya mnamo Disemba 31 mwaka huu, amekuwa akitangamana na mashabiki wake wa Kenya kwenye mitandao ya kijamii na hivi majuzi alimzawadia mmoja wao kwa kujibu swali kadiri ya matarajio yake.

 Mwimbaji huyo alishiriki video kwenye mtandao wa kijamii, ambapo alishiriki kipande cha moja ya nyimbo zake na kuwataka wafuasi wake kuitaja.

Aliahidi kutuma pesa kwa mtu wa kwanza ambaye  angeitambua  sawasawa.

 Shabiki wa Kenya ndiye aliyebahatika kushinda, ambaye aliutambua wimbo huo kwa usahihi na akatoa maoni yake kuhusu chapisho la Shusho.

 Kisha Shusho alimtumia KSh 1,000 kupitia M-Pesa na kushiriki picha ya skrini ya shughuli hiyo kwenye akaunti yake ya X.

"Nilimpa shabiki wangu kiamsha kinywa kwa kunipa jibu sahihi kwa swali langu,"Shusho aliniukuu.

View Comments