In Summary

• Olomide aliwapunga wengi bada ya kuingia jukwaani akiwa aemvalia viatu vyenye visigino virefu, ambavyo aghalabu huusishwa kuwa vya wanawake.

Koffi Olomide
Image: Facebook

Baada ya ngoja ngoja ya muda mrefu, hatimaye tamasha kubwa la Koffi Olomide lililokuwa linasubiriwa kwa kiu cha ajabu liifanyika Jumamosi katika ukumbi wa ASK Dome, jijini Nairobi.

Kama kawaida yake, mkongwe huyo wa miziki ya humba kutokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hakuweza kuwaangusha au kukatisha hamu ya mashabiki wake kwani alifanya kweli katika muda wa saa mbili na sekunde 35 aliotengewa jukwaani.

Mashabiki wake waliofurika waliweza kufurahia burudani la aina yake huku Olomide akiimba nao wimbo baada ya mwingine kwa mbwembwe za kufunga mwaka.

Kando na tumbuizo hilo la nguvu, mashabiki pia walivutiwa na chaguo la fasheni ya mavazi aliyovaa Olomide, wengi wakimsifia kwa kuwa na ladha nzuri ya fasheni licha ya kuwa ni mzee kiumri.

Olomide aliwapunga wengi bada ya kuingia jukwaani akiwa aemvalia viatu vyenye visigino virefu, ambavyo aghalabu huusishwa kuwa vya wanawake.

Kutoka juu mpaka chini alikuwa amevalia suti aina ya mauve yenye rangi ya pink kichwani akiwa amevaa kofia nyeupe yenye nembo ya bendera ya taifa la DRC lakini pia miguuni alikamilisha muonekano wake maridhawa na viatu hivyo vilivyozua gumzo mitandaoni wikendi.

Alipopanda jukwaani kutumbuiza nyimbo zake zilizovuma, mashabiki wa Koffi Olomide waliimba pamoja na nyimbo zake huku akifanya kweli jukwaani. Mwimbaji huyo wa Kongo alitoa onyesho la kuvutia, akiwaacha mashabiki wakishangaa na kummiminia sifa kwa wakati huo huo.

Licha ya umri wake kusonga, Olomide anajulikana na wengi kama msanii mwenye kiuno chepesi kwa kusakata densi na aliweza kulithibitisha hilo mbashara kwa wengi ambao mara nyingi humuona akifanya hivyo kwenye video za nyimbo zake.

“Asante, Kenya,” alichapisha kwenye akaunti zake za kijamii Jumapili baada ya shoo ya kihistoria iliyofanyika usiku wa Jumamosi.

View Comments