In Summary

• Cha kushangaza, Fella alifichua kwamba si yeye aliyemtafuta Diamond kufanya kazi na yeye bali Diamond ndiye alimtafuta kufanya kazi na yeye.

Mkubwa Fella.
Image: Screengrab

Meneja wa kazi za Sanaa za msanii Diamond Platnuzm, Mkubwa Fella amefunguka jinsi walikutana na msanii huyo kwa mara ya kwanza na kuwa na makubaliano ya kufanya kazi pamoja kama meneja wake.

Fella ambaye alikuwa anazungumza katika kipindi cha The Switch ndani ya Wasafi FM alifichua kwamba walipokutana, hakukuwa na maelewano kimkataba bali walikubaliana kwa maneno ya mdomo tu, na mpaka sasa hivi bado hawana mkataba baina yao unaoonesha kuwa wanafanya kazi pamoja bali ni makubalioano ya mdomo tu.

“Zamani hakuna maandishi baba asikuongopee mtu, zamani kukubaliana tu, na halafu hakuna mkataba mzuri kama kukubaliana, kuliko hata makaratasi yenu. Mkikubaliana inakuwa kama imetoka kwa dhati hiyo, hata ndio maana mpaka sasa hivi mimi nafanya kazi na Naseeb [Diamond Platnumz], sina hata karatasi moja ya kusema tumekubaliana na Diamond kufanya kazi, tofauti na wengine kuweka makaratasi mbele, uongo huo, kama hamjakubaliana kazi bure,” alisema Fella.

Aidha, Fella alirudisha akrabu nyuma kwa kusimulia jinsi walivyokutana na Diamond Platnumz na kuelewana kufanya kazi pamoja kama meneja na msanii.

Cha kushangaza, Fella alifichua kwamba si yeye aliyemtafuta Diamond kufanya kazi na yeye bali Diamond ndiye alimtafuta kufanya kazi na yeye.

Akijitambua kama staa mkubwa siku hizo, Mkubwa alisema kwamba ilimchukua Diamond Zaidi ya miezi mitatu kumfuata akimbembeleza ili kukubali kuwa meneja wa kazi zake za Sanaa.

“Diamond alinifuata, alisumbuka sana. Wakati ule ujue mimi ndio staa, alisumbuka sana kwa kweli kunitafuta. Sio kwamba eti kaja pale na kuniambia eti nikakubali kesho yake, hamna. Alikaa kama miezi 3, alisumbuka kidogo mpaka nikakuja kukubali yaani kidogo kataabika, sijui umenielewa?” alisema.

View Comments