In Summary

• Omari pia anasisitiza kwamba mteja wake ni mtumishi wa Mungu ambaye muda wote saa 24 kwa siku 7 za wiki anajitolea kumtumikia Mungu.

Omari na Embarambamba
Image: HISANI

Wakili wa msanii Embarambamba, Danstan Omari ameiandikia bodi ya KFCB barua ya kulalamikia matakwa na masharti makali ambayo walimpa msanii huyo kufuatia taharuki iliyotokea na wimbo wake mpya ‘Niko Uchi’.

Katika barua hiyo, Omari analalamika kwamba msanii huyo hakuwa analenga watu ambao wanalalamika kuhusu maudhui yake katika wimbo huo, bali lengo lake lilikuwa ni kuwafikia viziwi na ujumbe wake.

Omari pia anasisitiza kwamba mteja wake ni mtumishi wa Mungu ambaye muda wote saa 24 kwa siku 7 za wiki anajitolea kumtumikia Mungu na hivyo madai yanayoibuliwa kwamba maudhui yake ni ya kupotosha jamii si kweli.

“Mteja wangu ni mtumishi wa neno la Mungu na kazi zake za kibunifu siku zote amekuwa akizifanya kama kumtumikia Mungu na kuwavutia wengi kwa wokovu. Inashangaza kwamba badala ya kumpongeza mteja wangu kwa ubunifu alio nao, mumeamua kumkashifu na kumuua moyo kwa kumpa matakwa ya siyo sahihi,” sehemu ya barua hiyo iliyoonwa na radiojambo.co.ke ilisoma.

“Niko Uchi ni moja kati ya kazi zake za kibunifu ambazo zililenga kuwafikia viziwi ambao hawana uwezo wa kusikia ujumbe wake lakini bado wanaweza kuelewa ujumbe wake kutokana na kuona picha na video ya wimbo,” Omari aliongeza.

Wakili huyo maarufu pia alilalamikia kiasi cha faini ya milioni 6.4 ambazo KFCB inadaiwa kumtaka Embarambamba kulipa, akisema kwamba jambo hilo limemkosesha Amani kwani kama wanavyojua, Embarambamba kama wenzake hawajakuwa wakipokea mirahaba mizuri kutoka kwa bodi ya hakimili, MCSK.

“Mteja wetu, kama tu wasanii wengine nchini Kenya, anapokea mirahaba michache kutoka kwa MCSK, ukweli ambao pia nyinyi mnauelewa. Kutokana na hilo, mteja wetu ako katika hali ngumu ya kupata mamilioni ya fedha ambazo mlimtoza kama faini.”

View Comments