In Summary

• Licha ya kusema tu bila kuonekana kuwadunisha wenzake, baadhi ya washikadau wa Sanaa ya muziki kutoka Tanzania walihisi kwamba msanii huyo alisema kwa kuwabeza wasanii wenza.

Msanii wa kizazi kipya Otile Brown katika mahojiano ndani ya Radio Jambo.
Image: Radio Jambo (Facebook)

Msanii Otile Brown anazidi kutikisa vichwa vya habari ndani na nje ya Kenya kufuatia msururu wa mahojiano yake katika media mbali mbali.

Mahojiano yake ya hivi karibuni na mkuza maudhui Oga Obinna kwenye chaneli yake ya YouTube yamevutia hisia mseto huku msanii huyo akionekana kueneza chokoza chokoza zake kwa wasanii wenza kutoka nchi jirani ya Tanzania.

Msanii huyo alidai kwamba kwa pesa ananozipata humu nchini, akaenda nchini Tanzania ataishi kama mwana wa mfalme kwenye kasri kubwa la ajabu.

Brown alisema kwamba kwa kiasi cha hela anazolipa kwenye nyumba ya kupanga anayoishi hapa nchini, akachukua kiasi hicho na kuenda kupangisha nyumba nchini Tanzania, basi atapata jumba bora mithili ya kasri la kifalme.

“Mimi pengine nyumba ambayo ninalipa kodi hapa Kenya, pesa hizo za kodi, kama ningekuwa Tanzania ningekuwa naishi kwenye kasri,” msanii huyo alisema huku Obinna akimuliza kama upatikanaji wa nyumba Tanzania ni bei nafuu.

Licha ya kusema tu bila kuonekana kuwadunisha wenzake, baadhi ya washikadau wa Sanaa ya muziki kutoka Tanzania walihisi kwamba msanii huyo alisema kwa kuwabeza wasanii wenza.

Awali, Otile aligonga vichwa vya habari katika mahojiano hayo baada ya kudai kwamba hakuna msanii hata mmoja kutoka ukanda wa Afrika Mashariki mzima ambaye amefikia viwango vya kimataifa.

Otile alisema si hata Diamond ambaye amefikia viwango hivyo licha ya kuchukuliwa kuwa msanii aliyetusua Zaidi kimataifa.

Itakumbukwa hii si mara ya kwanza kwa Otile kuwachokoza wenzake kutoka Tanzania.

 Kipindi Fulani nyuma, Otile alikejeli cheni za wasanii Diamond na Mbosso ambazo walisema ni dhahabu ya bei ghali akisema kwamba vilikuwa vito ghushi tu.

View Comments