In Summary

• Akiwa jukwaani, Pozee alionekana kuwa na kijikaratasi kilichosokotwa mfano wa sigara ambacho alikiwasha kwa kutumia kiberiti.

WILLY PAUL
Image: INSTAGRAM

Msanii wa kizazi kipya Willy Paul amekanusha madai kwamba anatumia pombe na dawa za kulevya kama bangi.

Akizungumza na waandishi wa habari ya burudani baada ya kumaliza kutumbuiza kwenye shoo ya Boom Fest wikendi iliyopita, Willy Paul alifunguka kuhusu tukio alilolifanya jukwaani pamoja na wacheza densi wake.

Akiwa jukwaani, Pozee alionekana kuwa na kijikaratasi kilichosokotwa mfano wa sigara ambacho alikiwasha kwa kutumia kiberiti, jambo lililowafanya baadhi ya mashabiki wake kudhani kwamba alivuta bangi aliwa mubashara jukwaani.

Hata hivyo, Pozee kwa kuthibitisha kuwa sio bangi, alionesha kijikatarasi hicho na kiberiti akisema kwamba si bangi wala sigara kwani yeye katika maisha yake hajawahi tumia vitu hivyo.

“Hapana. Hapana! Sijawahi kunywa pombe, sijawahi vuta bangi. Ndio hii kitu tumefanya,” Pozee alisema huku akionesha kijikatarasi hicho na kiberiti, “Hii ni karatasi, ilikuwa tu ya kutengeneza shoo, ilikuwa ni ya kuchanganya watu.”

Msanii huyo alienda mbele na kuapa kwa jina la mama yake kwamba katika maisha yake hajawahi tumia kileo chochote.

“Katika jina la Yesu, mimi sijawahi kunywa pombe sijawahi vuta bangi, wallahi mama yangu. Mimi ni mtu tofauti na ndio maana umeona nimetumbuiza kushinda wasanii wengi,” alisisitiza.

“Nina njia nyingi za kufanya mambo yangu lakini kukunywa kwa kweli hapana,” aliongeza.

Msanii huyo alizungumzia siri yake ya kudumu kwenye muziki kwa muda mrefu akisema ni kwa jitihada zake mwenyewe, maombi ya mama yake na mashabiki wake kindakindaki lakini pia kushikiliwa na Mungu.

Akizungumzia kitu ambacho alikuwa anakiogopa kabisa, Pozee alisema,

“Woga pekee ambao niliwahi kuwa nao ni kurudi katika yale maisha mabaya ambayo nilikuwa nayo zamani, lakini nilishinda woga huo, Mungu amekuwa mwema kwangu.”

View Comments