In Summary

• Baba huyo wa watoto 4 kutoka kwa kina mama tofauti katika mahojiano aliweka wazi kwamba kazi ya malezi ya watoto si rahisi, haswa watoto wanaokaribia umri wa baleghe.

Obinna na mwanawe
Image: Instagram

Mkuza maudhui Oga Obinna ameweka wazi kuhusu baadhi ya sheria na masharti ambayo anatumia kuwalea wanawe.

Baba huyo wa watoto 4 kutoka kwa kina mama tofauti katika mahojiano aliweka wazi kwamba kazi ya malezi ya watoto si rahisi, haswa watoto wanaokaribia umri wa baleghe.

Obinna alisema kwamba ili kuhakikisha hawapotoki katika kizazi hiki chenye urahisi wa kufikia kila kitu kupitia utandawazi, amewapiga marufuku kufanya baadhi ya mambo ikiwemo kusikiliza miziki aina ya Gengetone na Arbantone.

“Katika nyumba yangu kuna sheria kwa sababu bila sheria kutakuwa na visa vya utovu wa nidhamu. Wanangu kuna baadhi ya vitu hawawezi tazama kwa runinga, wanajua hilo. Kwa mfano miziki ya Gengetone kwa nyumba yangu hawawezi sikiliza, pia Arbantone. Lakini mimi husikiliza miziki hiyo na ninaweza tunga miziki hiyo na wanangu wanajua,” Obinna alisema.

Mkuza maudhui huyo ambaye pia ni mtunzi wa nyimbo alisema kwamba ni jukumu lake kama mzazi kuchunga baadhi ya vitu vinavyowafikia wanawe, akisisitiza kwamba hana chuki dhidi ya wasanii wa Gengetone na Arbantone.

Pia alisema kwamba mwanawe wa kiume ambaye amefikisha umri wa miaka 14 siku chache zilizopita amekuwa akifuatilia simulizi za aliyekuwa mwanahabari wa Citizen TV, Kimani Mbugua kama njia moja ya kujifunza kwamba kuna baadhi ya maamuzi katika maisha akifanya ataishia katika maisha Fulani ambayo si mazuri.

“Mimi huwa naketi chini na wanangu na nawaeleza kwamba kuna baadhi ya vitu ukifanya, hili na lile litakupata. Hata video ya Kimani Mbugua, mwanangu wa kiume amekuwa akiitazama ili ajifunze. Huwa namwambia kama utachagua njia kama hii, hili linaweza likakupata,” Obinna alisema.

Itakumbukwa wiki iliyopita, Obinna kwa kushirikiana na wahisani wema pamoja na babake Kimani, walimuokoa kutoka mtaani na kuahidi kumpeleka katika kituo cha kurekebisha tabia katika kile kilitajwa kuwa kijana huyo ameathirika kiakili, haswa kwa kuzingatia vitu ambavo amekuwa akivifanya na kuvisema kwenye mitandao ya kijamii siku za hivi majuzi.

View Comments