In Summary

• Diamond alidai kwamba katika wanaume hao wanaomtongoza Zuchu kwenye DM, baadhi ni wasanii maarufu wa Bongo Fleva.

Zuchu na Diamond
Image: Facebook//Zuchu

Msanii Diamond Platnumz ameapa kuwaanika hadharani wanaume wanaojipendekeza kwa mpenzi wake Zuchu kupitia DMs zake.

Kwa mujibu wa msanii huyo bosi wa lebo ya WCB Wasafi, anatathmini kupiga hatua hiyo ya kuwaanika hadharani baada ya kuchoka kuvumilia kuona jinsi wanaume wanajimaliza na mistari yao kumtongoza Zuchu kwenye DM.

Diamond alidai kwamba katika wanaume hao wanaomtongoza Zuchu kwenye DM, baadhi ni wasanii maarufu wa Bongo Fleva.

Diamond alisema kwa kujiamini kwamba ana ushahidi tosha kwani amekuwa akichukua screenshot za jumbe hizo za wanaume wanaojipendekeza kwenye DM za Zuchu, na anatazamia kuzichapisha zote kama njia moja ya kuwakomesha na kusimika Zaidi uhusiano wake na binti huyo ambaye pia ni msanii chini ya lebo yake.

“Tutaanza kuzichapisha meseji zao kwa sababu kama mimi nina screnshots za kutosha tu. Nataka nianze kuwaanika wanaomnyapia Zuhura[Zuchu],” Diamond alitoa mkwara.

Haya yanajiri siku chache baada ya wawili hao kuachia wimbo wao wa kolabo baada ya kuonekana kutupiana vijembe kwenye mitandao ya kijamii.

Wengi walidhani kwamba Diamond na Zuchu wamefikia kikomo cha mapenzi yao wiki chache zilizopita baada ya wawili hao kusitisha urafiki kwenye mtandao wa Instagram, chanzo kikitajwa kuwa mpenzi wa zamani wa Diamond.

Diamond awali akitumbuiza kwenye  tamasha moja, alimtambulisha kwa kumkaribisha kwenye jukwaa, mrembo kwa jina Sarah, ambaye alidai alikuwa mpenzi wake miaka 15 iliyopita.

Msanii huyo mwenye maisha changamano ya kimapenzi alieleza kwamba mrembo huyo ndiye alimfanya kuandika wimbo wa ‘Kamwambie’ baada ya juhudi zake za kumtaka kimapenzi kugonga mwamba.

Hilo lilitajwa kuwa chimbuko la ugomvi wake na Zuchu aliyearifiwa kufungasha virago na kuondoka, lakini wengi walishangaa kuona wako pamoja baada ya kuachia wimbo, na kuwaaminisha baadhi kwamba matukio yote ya nyuma yalikuwa yameratibiwa ili kufukuzia upepo kwa ajili ya dude lao jipya.

View Comments