In Summary

• “Sasa hivi niko afadhali kidogo, ninaishi Kasarani. Sasa hivi niko na kwangu na maisha hayako sawa vile lakini naweza sema ninajaribu,” aliongeza.

STEVO SIMPLE BOY.
Image: Instagram

Rapa mwenye misemo mingi, Stevo Simple Boy amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu maisha yake kama msanii huru, miezi michache baada ya kutengana na aliyekuwa meneja wake.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani, msanii huyo alifichua kwamba kwa sasa angalau ameanza kuona mwanga japo kwa mbali, akisema kwamba amebadilisha mazingira yake kutoka mtaa duni wa Kibera kwenda Kasarani.

Ikumbukwe miezi michache baada ya kutengana na aliyekuwa meneja wake, uvumi uliibuka kwamba msanii huyo alilazimika kurejea mtaani Kibera baada ya kuondoka katika nyumba iliyokuwa inalipiwa na uongozi wake mtaani Buruburu.

“Kwa sasa maisha ni angalau, tangu niwe meneja na niwe na timu yangu. Naweza sema angalau mambo yanakwenda sawa, shoo zinakuja kidogo kidogo, na madili pia yanakuja. Kwa hivyo natumai mambo yatakuwa sawa Zaidi hivi karibuni,” Stevo alisema.

“Sasa hivi niko afadhali kidogo, ninaishi Kasarani. Sasa hivi niko na kwangu na maisha hayako sawa vile lakini naweza sema ninajaribu,” aliongeza.

Mapema mwaka huu, Stevo na aliyekuwa meneja wake, Chingiboy Mstado walivurugana baada ya meneja huyo kudai kwamba msanii huyo alikuwa anafanyiwa maamuzi kuhusu kazi yake na familia yake.

Chingiboy alisema kwamba baadhi ya wanafamilia wa Stevo walikuwa wanaingilia majukumu yake kiasi kwamba ilibidi achukue uamuzi wa kumuacha ili asimamiwe na familia.

Chingi aliibua madai kwamba mmoja wa wanafamilia wa Stevo alikwenda katika nyumba ambayo uongozi ulikuwa unalipia na kumhamisha hadi Kibera, jambo lililokwamisha uhusiano wao.

Meneja huyo alikwenda mbele na kushikilia akaunti za mitandao ya kijamii za msanii huyo, akitaka fidia ya pesa alizotumia kukomboa akaunti hizo kutoka kwa uongozi wa awali.

Hata hivyo, baada ya vuta nikuvute, Chingi alifanya uungwana na kuachilia akaunti hizo kwa Stevo bila kumdai hata senti, wiki chache baadae.

 

View Comments