In Summary

• Mtangazaji huyo wa kipindi cha Asubuhi alisema kwamba matokeo duni kwenye KCSE hayafai kutumiwa kama kigezo cha kuamua kuwa mtu hana uelewa kaitka jambo Fulani.

GIDI

Saa chache ya waziri mteule wa madini na uchumi wa baharini, Ali Hassan Joho kufafanua bayana kuhusu kiwango chake cha elimu, watu mbalimbali mitandaoni wamejitongeza kuunga mkono kauli za gavana huyo wa zamani wa Mombasa.

Joho alifichua kwamba alipata alama ya D- kwenye mtihani wake wa shule ya upili lakini hilo halikumzuia kujiendeleza kimasomo na kubadilisha matokeo na mustakabali wa maisha yake.

Gavana huyo wa zamani alifichua kwamba kwa sasa ana digrii mbili na pia yuko mbioni kupata PhD yake.

Kauli hizi zilimsisimua mtangazaji wa Radio Jambo Gidi Ogidi ambaye alichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook akikiri kukubaliana na Joho kwamba matokeo ya KCSE kamwe hayafai kutumiwa kama kigezo kuhukumu mustakabali wa maisha ya mtu.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha Asubuhi alisema kwamba matokeo duni kwenye KCSE hayafai kutumiwa kama kigezo cha kuamua kuwa mtu hana uelewa kaitka jambo Fulani.

“Nakubaliana na Joho, matokeo ya masomo ya shule ya upili hayafai kamwe kutumiwa kufafanua au kulaani uwezo wa mtu maishani. Matokeo duni katika shule ya upili haimaanishi ukosefu wa akili au uwezo.”

“Kwa kweli, baadhi ya watu wanaotatizika kielimu katika shule ya upili huendelea kupata mafanikio ya ajabu katika biashara na maeneo mengine ya maisha. Mitihani ya shule ya upili inawakilisha kiwango cha msingi cha elimu na sio kipimo cha mwisho cha uwezo wa mtu au uwezo wake wa baadaye,” Gidi alisema.

Gidi akitetea kauli yake alisema kwamba baadhi ya wanafunzi hupitia changamoto nyingi za kimaisha wakati wa mitihani ya kitaifa hivyo kuathiri matokeo yao, hivyo haipaswi kutumiwa kupima uwezo wao wa kimaisha.

“Wanafunzi wengi pia mara nyingi hukumbana na hali nyingi zenye changamoto wakati wa mitihani ya shule ya upili, kama vile ugonjwa, mazingira magumu ya mitihani, au maswala ya kifamilia, mafadhaiko n.k ambayo yanaweza kuathiri matokeo yao. Haimaanishi kuwa hawana uwezo,” aliongeza.

View Comments