In Summary

•Diana Marua amekiri kuridhishwa na mahaba mazito anayopata kutoka kwa mumewe, mwanamuziki Kelvin Kioko almaarufu Bahati.

•Diana alifunguka kuhusu wapenzi wawili wa zamani ambao alikuwahi kuwa katika hali ya kutoelewana nao kuhusu masuala tofauti.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu Diana Marua amekiri kuridhishwa na mahaba mazito anayopata kutoka kwa mumewe, mwanamuziki Kelvin Kioko almaarufu Bahati.

Katika video ya hivi majuzi kwenye chaneli yake ya YouTube, mama huyo wa watoto watatu alidokeza kwamba amefurahishwa sana na hatua ya mumewe ya hivi majuzi ya kumvisha pete ya uchumba kiasi kwamba yuko tayari kumruhusu mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo afanye lolote bila kumhoji.

“Kupendwa raha jamani. Saa hii hata Bahati akifanya kitu na nisikie ni kama nataka kukasirika, nakumbuka aliweka pete katika kidole changu siku chache zilizopita na mimi nasema ni sawa, ni sawa mpenzi unaweza kufanya chochote unachotaka,” Diana Marua alisema. .

Rapa huyo alifunguka kuhusu jinsi anavyojawa na furaha baada ya mzazi huyo mwenzake mwenye umri wa miaka 30 kumchagua kati ya wanawake wote aliowahi kuwa kwenye mahusiano nao.

“Jamani, mnaweza kufikiria tu kuhusu kuchumbiwa? Mpenzi wako anakuja kwako na kukuambia kuwa umewashinda wote. Mimi, nimewashinda wote?,” alihoji.

Diana Marua pia alitumia fursa hiyo kuwarushia vijembe wapenzi wake wa zamani ambao walimtendea vibaya wakati wa uchumba wao.

Alifunguka kuhusu wapenzi wawili wa zamani ambao alikuwahi kuwa katika hali ya kutoelewana nao kuhusu masuala tofauti.

“Wale machali walinimistreat tukidate. Yule chali alikuja kuniambia wewe hujui kupika, enda upate mafunzo ya kupika na hayo yote,” Diana alisimulia.

“Yule chali alinitesa, Yule chali mwenye siku moja tulikasirikiana, akienda job akanidrop mahali. Nikafungua mlango wa gari akaendesha kama sijashuka gari nikaanguka hapo chini, ona Mungu wangu.”

Mke huyo wa Bahati alibainisha kuwa Mungu amemtendea mengi na kumkomboa kutoka katika maisha ya mateso.

“Ona Mungu wangu, ona jumba, ona maisha yangu, angalia magari ninayoendesha. Siringi ama chochote. Ni msaada wa Mungu na amenitendea. Nitasema hayo kumsherehekea Mungu kwa sababu nimeteseka huko nyuma. Nahisi nimebarikiwa,” Diana alisema.

Mapema mwaka huu, wapenzi hao mashuhuri walipeleka mahusiano yao katika hatua nyingine baada ya Bahati kumchumbia mwanavlogu huyo kwa mara ya pili.  Wawili hao walirekodi kipindi hicho kizuri katika video iliyopeperushwa kwenye chaneli ya YouTube ya Diana Marua takriban wiki mbili zilizopita.

Wakati akichukua hatua hiyo kubwa, Bahati alibainisha kuwa amekamilisha hatua zote muhimu kuelekea ndoa na sasa yuko tayari kuifanya rasmi. Baadaye, msanii huyo alitangaza tarehe 12 Desemba kuwa siku ya harusi yao.

View Comments