HAPANA! Wenye magari wapinga NTSA kuhusu ukaguzi wa magari ya kibinafsi
Muungano wa wenye magari nchini (KMA) umepinga vikali pendekezo la maamlaka ya usalama barabarani NTSA la kuanza ukaguzi wa magari yote ya kibinafsi . Kupitia taarifa kali yenye lalama nyingi kuhusu pendekezo hilo ,mwenyekiti wa muungano huo Peter Murima amedai kwamba hatua hiyo imechochewa na uchu wa serikali kujipa mapato badala la usalama wa magari hayo .Murima amesema tayari wenye magari ya kibinafsi wanatozwa kodinzito na nyingi kwa kuyatumia magari yao ilhali barabara kote nchini ni mbovu .
Maamlaka ya NTSA wiki jana ilichapishwa mswada wa mwongozo unaopendekeza na kutoa kanuni za jinsi magari yote yatakavyokaguliwa ili kudumisha usalama barabarani . Katika mapendekezo hayo ,NTSA itakuwa na maamlaka ya kuwapa ruhusa wafanyibiashara wa kibinafsi kufungua vituo vya kuyakagua magari . Tayari NTSA imeanza kufanya vikao vya umma kuhusu mapendekezo yake .
KMA imesema hatua hiyo ya serikali inalenga kuzidisha ufisadi ambao huambatana na zoezi zima la kuyakagua magari ya usafiri wa umma nay ale ya kibiashara . Murima ,katika taarifa yake ameshangaa jinsi serikali ilivyokosa haya kwa kutaka kutwika mzigo zaidi wenye magari ilhali tozo ya utunzi na ukarabati wa barabara imeongezwa kwa kutoska shilingi 8 hadi shilingi 24 ndani ya kipindi cha miaka miwili .Amesema serikali kwanza inafaa kuziimarisha barabara zote nchini kabla ya kutekeleza pendekezo la ukaguzi wa magari ya kibinafsi .