David Luiz: Defenda wa Arsenal asema kushindwa kwao mabao 3-0 na Mancity ni kwa sababu ya makosa yake
Mlinzi wa kilabu ya arsenal David Luiz amekubali kuwajibikia kushindwa kwao mabao 3 kwa nunge na Manchester City lakini akasema yungali ana matumaini ya kuichezea kilabu hiyo.
Luiz, ambaye mkataba wake unatamatika mwishoni mwa mwezi huu aliondolewa uwanjani ili kutamatisha kurejea kwake uwanjani kuliozongwa na makosa chungu nzima .
"Ni makosa yangu, timu ilifanya vyema hasa ikiwa na wachezaji 10 kocha pia yuko sawa na yote ni kwa ajili ya makosa yangu" amesema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33.
"Nataka kusalia hapa. Kocha anafahamu hilo ma anataka nisalie hapa."
Luiz alijiunga na Arsenal kipindi kilichopita cha uhamisho kutoka Chelsea kwa pauni milioni 8 na alikuwa ameachwa katika benchi dhidi ya City kwa ajili ya kutoeleweka kuhusu hali ya mkataba wake.
Aliingia uwanjani katika dakika ya 24 baada ya kujeruhiwa kwa Pablo Mari na alifanya masihara yaliompa bao la kwanza Raheem Sterling.
Kisha baadaye alihusika na kumbwaga chini Riyad Mahrez na kusababisha penalty na kuonyeshwa nje ya uwanja. Kufurushwa kwake kutoka mechi hiyo kunamaanisha ameichezea arsenal mchuano wake wa mwisho endapo hatazidisha mkataba wake.