Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewataka watanzania kutenga muda na kujiunga na wakenya kuombea janga la virusi vya corona.
Magufuli siku ya Ijumaa aliwaambia watanzania kwamba kama tu vile walimuomba Mungu kuwaondolea Corona, wakati umewadia kwa wao kujiunga na wakenya ambao wana uhusiano wa karibu nao kuomba pamoja.
Magufuli alikuwa akizungumza katika mkutano wa kampeini wa chama cha Mapinduzi katika uwanja wa Benjamin Mukapa mjini Dar es Salaam.
"Miezi michache iliyopita nchi yetu ilikuwa miongoni mwa zile zilizokuwa zimeathirika na Coronavirus, tuliketi na viongozi wa kidini na kuomba Mungu ailinde nchi yetu. Twamshukuru Mungu kwa sababu kwake hakuna jambo gumu alitusaidia kushinda ugonjwa," Magufuli alisema.