In Summary
  • Tunai asafirishwa Nairobi kwa matibabu baada ya helikopta aliokuwa ameabiri kuanguka
  • Video yaonyesha vile helikopta hiyo ilianguka baada ya kupata ugumu kupaa angani 

 Gavana wa Narok Samuel Tunai aliponea kifo baada ya ndege aina ya helikopta aliokuwa ameabiri kuanguka ilipokuwa inajiandaa kupaa angani.

Kulingana na video inayoonyesha matukio kabla na baada ya ajali hiyo, ndege hiyo mwanzo ilikuwa na ugumu kupaa huku rubani akilazimika kutua mara mbili kabla ya kujaribu kupaa na kisha ikaanguka sekunde chache baadaye kabla haijapaa juu zaidi.

Wananchi waliokuwa wamejitokeza  kumuaga gavana wao walifanya juhudi kuokoa waliokuwa ndani ya ndege hiyo, na gavana huyo na wengine waliokuwa ndani wakapandishwa katika ambulansi na kupelekwa hospitalini kufanyiwa uchunguzi na madaktari.

 

 
 

Msemaji wa serikali ya kaunti ya Narok, Paul Tobiko alisema kwamba waliokuwa katika ndege hiyo ni gavana Tunai, msaidizi wake na rubani.

"Ingawa visa kama hivyo huleta wasiwasi mkubwa, serikali ya kaunti ya Narok ingependa kuwahakikishia kuwa hakukuwa na majeraha makubwa," Tobiko alisema.

Msemaji huyo wa kaunti aliwahakikishia wananchi wa Narok kwamba gavana wao yuko salama na atarejea kazini hivi karibuni. 

(Mhariri Davis Ojiambo)

View Comments