In Summary

•Wakili wa mshukiwa alimtetea kwa kusema kuwa marehemu aliaga katika harakati ya kupewa nidhamu kufuatia matendo yake mabaya.

•Jaji alisema kuwa Ndung'u alifaa kupata hukumu kali ili awe funzo kwa wanaochukua sheria mikononi mwao.

court

Jamaa mmoja amehukumiwa kifungo cha miaka 40 gerezani baada ya kupiga na kuchoma mshukiwa wa wizi wa ng'ombe.

Inadaiwa kuwa Samwel Ndung'u Wainana akishirikiana na wengine ambao hawakutambulishwa walimtesa, kumpiga kisha kumchoma mtu aliyetuhumiwa kuiba ngomb'e pande za Nyahururu.

Inasemekana kuwa walivunja mguu wa marehemu kisha wakaushika na kumvuruta kabla ya kumteketeza. 

Ndung'u haswa ameshtakiwa kuwa alimtesa marehemu kwa kumchoma usoni kwa kutumia kiwavi na kuwekelea gurudumu kwenye shingo lake.

Katika hukumu yake tarehe siku ya Jumatatu, Jaji Charles Kariuki wa mahakama kuu ya Nyahururu alisema kuwa marehemu alifaa kupewa kifungo cha maisha kwa kuiba ng'ombe iwapo angefikishwa mahakamani na kuhukumiwa.

Alisema kuwa Ndung'u alifaa kupata hukumu kali ili awe funzo kwa wanaochukua sheria mikononi mwao.

Wakili wa mshukiwa alimtetea kwa kusema kuwa marehemu aliaga katika harakati ya kupewa nidhamu kufuatia matendo yake mabaya.

"Mshukiwa amegundua kuwa ilikuwa hatia kuchukua sheria mikononi kwa kumfunza nidhamu marehemu, tendo ambalo lilisababisha kifo chake" Wakili alisema na kuagiza mahakama kumuelewa mshukiwa.

Hata hivyo, mahakama ilithibitisha kuwa mshukiwa alikuwa na rekodi mbaya ya uhalifu.

Mahakama ilipoagiza uchunguzi kuhusiana na rekodi ya mshukiwa, alikataa kushirikiana na wapelelezi na kwa hivyo ripoti haingewezwa kutayarishwa.

Jaji Kariuki alisema kuwa mshukiwa alitenda kitendo kisicho cha utu na kukiuka haki za kibinadamu. Alisema kuwa mshukiwa alisababisha uchungu mwingi kwa marehemu kabla ya kufariki kwake.

View Comments