In Summary

•Mshukiwa huyo ambaye ana umri wa miaka 22 alipatikana akilamba damu ya mwili wa aliyekuwa mwalimu katika shule ya  msingi ya Gul Kagembe iliyo maeneo ya Rangwe.

•Ndugu ya marehemu, Wycliffe Onyango, alieleza  Mpasho kuwa mshukiwa  alipokamatwa alijaribu kuhonga mhudumu wa mochari ila akakataa na kuarifu wengine.

crime

Kweli dunia ina mambo na vijimambo!

Mwanaume mmoja anazuiliwa katika kituo cha cha Homabay baada ya kupatikana akilamba damu ya maiti katika chumba kimoja cha kuhifadhi maiti kaunti hiy.

Mshukiwa huyo ambaye ana umri wa miaka 22 alipatikana jioni ya Alhamisi akilamba damu ya mwili wa aliyekuwa mwalimu katika shule ya  msingi ya Gul Kagembe iliyo maeneo ya Rangwe.

Clinice Atieno Ojenge, 40, ambaye alikuwa mwalimu katika shule ya chekechea alipigwa risasi pamoja na bintiye wa miaka 9  na watu wasiojulikana mnamo Juni 15. Walivamiwa katika boma lao katika kijiji cha Koyolo maeneo ya Rangwe.

Ripoti ya polisi inasema kuwa mshukiwa alifika kwenye chumba cha kuhifadhi maiti akiwa amebebwa na bodaboda na kusema kuwa anataka  kuona mwili wa jamaa wake. Aliruhusiwa kuingia na  kufuata kanuni zote za kuona mwili  kama alivyoagizwa baada ya kuonyeshwa mahali mwili ulikuwa.

Jambo la kushangaza ni kuwa alipokuwa anaelekea kwenye lango alisimama na kuanza kulamba damu kwenye mwili wa marehemu Atieno uliokuwa umelazwa pale.

Ndugu ya marehemu, Wycliffe Onyango, alieleza  Mpasho kuwa mshukiwa  alipokamatwa alijaribu kuhonga mhudumu wa mochari ila akakataa na kuarifu wengine.

"Mshukiwa alijaribu kuhonga mhudumu wa mochari ila akakataa na kuarifu wengine ndipo akakamatwa. Watu walitaka kumchoma. Mwanawe marehemu ambaye alinusurika kifo wakati wa mashambulizi yaliyoacha mamake akiwa maiti alimtambulisha mshukiwa kama mmoja wa waliohusika kwenye mashambulizi." Onyango alisema

Onyango alieleza kuwa magaidi wale hawakuchukua chochote kwenye nyumba ya marehemu. Alisema kuwa nia ya magaidi hao ilikuwa kuangamiza familia ya marehemu ila mtoto mmoja alinusurika bila majeraha huku aliyepigwa risasi akiendelea kuhudumiwa hospitalini.

View Comments