In Summary

•Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa  kumi jioni wakati gari la Toyota Wish nambari ya usajili KCN 490V lililokuwa likitoka upande wa mji wa Narok liligongana na gari aina ya matatu, nambari ya usajili ya KDA 746X lililokuwa likitoka upande huo mwingine.

•Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, dereva wa Toyota Wish alikuwa akijaribu kumkwepa mlevi ambaye alikuwa anavuka barabara wakati alipohusika kwenye ajali hiyo.

Mabaki ya magari ambayo Ilihusika katika ajali mbaya eneo la Maltaro kando ya barabara kuu ya Narok-Mai Mahiu.
Image: ANN SALATON

Watu wanne ikiwemo dereva na abiria watatu walifariki papo hapo baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Maltauro, kando ya barabara ya Narok-Maimahiu Jumapili.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa katika kaunti ya Narok John Kizito, ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa  kumi jioni wakati gari la Toyota Wish nambari ya usajili KCN 490V lililokuwa likitoka upande wa mji wa Narok liligongana na gari aina ya matatu, nambari ya usajili ya KDA 746X lililokuwa likitoka upande huo mwingine.

"Ilitokea kwamba dereva wa Wish (marehemu) aliyekuwa akiendesha gari kutoka Narok kuelekea Mai Mahiu, alipofika eneo la ajali alipita bila kujali na hivyo kugongana uso kwa uso na matatu iliyokuwa ikiendeshwa kutoka upande mwingine," Kizito alieleza.

Kutokana na ajali hiyo, bosi huyo wa polisi alisema, dereva wa Toyota Wish alifariki papo hapo pamoja na abiria wake wawili huku abiria mwingine wa kike aliyekuwa kwa matatu pia akiaga.

Alisema waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok kwa matibabu huku maiti nne zikiwa zimelazwa katika hifadhi ya maiti ya kituo hicho

"Eneo la tukio lilitembelewa na kufanyiwa kazi pamoja na mabaki ya magari yanayosubiri kuvutwa hadi kituoni kwa ukaguzi," alisema Kizito.

Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, dereva wa Toyota Wish alikuwa akijaribu kumkwepa mlevi ambaye alikuwa anavuka barabara wakati alipohusika kwenye ajali hiyo.

(Utafsiri: Samuel Maina)

View Comments