In Summary

•Hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa katika tukio hilo la usiku wa kuamkia Jumatatu huku mali ya mamilioni ya pesa ikiharibiwa.

•Masanduku na vitabu vilivyokuwa vimeteketea vilitapakaa nje ya mabweni wakati wanahabari walipowasili

Mzazi akibeba mabaki ya mali ya watoto wake wawili kutoka kwa vifusi katika shule ya bweni ya Sameta, Kisii Jumanne, Mei 17, 2022.
Image: MAGATI OBEBO

Moto mkubwa  uliteketeza mabweni mawili katika shule ya msingi ya Sameta, kaunti ya Kisii.

Hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa katika tukio hilo la usiku wa kuamkia Jumatatu huku mali ya mamilioni ya pesa ikiharibiwa.

Wanafunzi 82 waliokuwa wanalala katika mabweni yaliyoathiriwa waliweza kuponea bila majeraha.

Mwalimu mkuu Ibrahim Ondati hakuweza kubashiri kuhusu chanzo cha moto huo wakati wanahabari walipotembelea shule hiyo.

Bw Ondati hakuwepo shuleni wakati ambapo moto huo ulizuka mwendo wa saa moja usiku wa Jumatatu.

Aliwaelekeza waandishi wa habari kutembelea ofisi ya mkurugenzi wa elimu kwa maelezo zaidi.

Wazazi waliokuwa wamejawa na wasiwasi walisema walipokea simu wakifahamishwa kuhusu moto katika shule hiyo.

"Kila kitu katika eneo la tukio kimeharibiwa na moto kama unavyoona. Ni hasara kubwa lakini tuna furaha watoto wetu wako salama," alisema mama mmoja kwa mwanafunzi wa darasa la 7.

Masanduku na vitabu vilivyokuwa vimeteketea vilitapakaa nje ya mabweni wakati wanahabari walipowasili Jumanne alasiri.

Baadhi ya wazazi walionekana wakichukua watoto wao kwa magari.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Sameta Muroki Muyuri alisema ilikuwa bahati kuona hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

Hata hivyo wanafanya uchunguzi kubaini ikiwa mabweni yalichomwa na mtu. 

Moto huo ulizuka wakati hapakuwa na umeme shuleni, alisema.

"Tayari maafisa kutoka DCI wamezuru eneo la tukio na watafanyia kazi ripoti watakayotupa," alisema.

View Comments