In Summary

• Bei ya vyakula na bidhaa za kimsingi za walaji katika miezi ya hivi karibuni imekuwa katika hali ya juu huku gharama ya baadhi ya bidhaa za msingi ikipanda juu sana.

Unga wa mahindi ukiwa katika kabrasha la duka la kuuza kwa jumla
Image: The Star (Maktaba)

Ni habari njema kwa Wakenya haswa wapenzi wa sima baada ya serikali kutangaza kupunguzwa kwa bei ya unga wa ugali hadi shilingi 100.

Unga wa mahindi sasa utauzwa kwa Sh100 kuanzia leo (Jumatatu) kufuatia hatua ya serikali kutoa ruzuku kwa bei ya awali.

Kulingana na hati ya mawasiliano ya ndani iliyotiwa saini na katibu wa kudumu katika wizara ya Kilimo Francis Owino, Wizara itafadhili bei ya unga wa mahindi unaozalishwa na kuuzwa na wasaga mahindi kwa muda wa wiki nne.

Pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi sasa itauzwa kwa Sh100 chini kutoka Sh230.

"Bei ya reja reja inayopendekezwa ya unga isizidi Sh100 kwa pakiti ya kilo 2, Sh250 kwa pakiti ya kilo 5 na Sh490 kwa pakiti ya kilo 10." Barua hiyo ilieleza.

Barua hiyo inazidi kusema kuwa Wizara itapeleka wawakilishi wao kwenye majengo na bohari za msagaji ili kuthibitisha uthibitisho wa uuzaji wa unga wa mahindi sokoni.

Bei ya vyakula na bidhaa za kimsingi za walaji katika miezi ya hivi karibuni imekuwa katika hali ya juu huku gharama ya baadhi ya bidhaa za msingi ikipanda juu sana na kufanya maisha ya Wakenya kuwa magumu kupindukia.

Bei zilizoathirika zaidi ni za unga wa mahindi na ngano, sukari, mafuta ya kupikia, karatasi ya tishu, maziwa, mboga na mkate.

Utafiti uliotolewa wiki jana na kampuni ya utafiti ya Infotrak ulionyesha kuwa asilimia 73 ya wakaazi wa Nairobi wanahisi kuwa nchi inaelekea pabaya. Wengi wa walio na maoni haya (81%) walitaja gharama kubwa ya maisha kuwa sababu ya madai yao.

Gharama ya maisha nchini Kenya iliongezeka zaidi mwezi wa Mei kutokana na bei ya juu ya vyakula na mafuta kufikia asilimia 7.1 kutoka 6.47 mwezi Aprili na asilimia 5.556 mwezi Machi.

Data ya Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya (KNBS) Fahirisi ya Bei ya Watumiaji na Mfumuko wa bei ilionyesha kuwa kupanda kwa bei kulichangiwa zaidi na ongezeko la bei za bidhaa chini ya kapu la vyakula na vinywaji visivyo na kileo (asilimia 12.4).

View Comments