In Summary

•Siku ya Jumanne Mahakama ya Kikatiba ilimkuta Zuma na hatia ya kudharau agizo la mahakama la kuhudhuria kwenye kesi yake ya madai ya ufisadi na kumpa adhabu ya kifungo cha miezi 15 jela.

•Mkusanyiko huo wa wafuasi wa Zuma ni haramu kwa kuwa unavunja kanuni za kudhibiti ugonjwa wa corona, lakini hakukuwa na askari walioenda kuwaondosha watu. Hali hiyo imewafanya baadhi ya watu kuona kuwa kiongozi huyo yupo juu ya sheria kwa kuwa ana nguvu kubwa ya kisiasa.

Wafuasi wa Zuma wamekuwa wakikusanyika nje ya makazi yake kwa juma lote lililopita
Image: GETTY IMAGES

Wafuasi wa rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma wametengeneza kile wanachokiita 'ngao ya binadamu' nje ya nyumba yake ili kuzuia kiongozi huyo asikamatwe.

Siku ya Jumanne Mahakama ya Kikatiba ilimkuta Zuma na hatia ya kudharau agizo la mahakama la kuhudhuria kwenye kesi yake ya madai ya ufisadi na kumpa adhabu ya kifungo cha miezi 15 jela.

Bwana Zuma alipewa hadi usiku wa manane Jumapili kujisalimisha mwenyewe.

Hata hivyo, siku ya Jumamosi Mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini ilikubali kusikiliza ombi la Zuma la kutaka kifungo cha miezi 15 jela kifutiliwe mbali.

Haijulikani kama uamuzi wa mahakama wa kusikiliza rufaa dhidi ya uamuzi wake wenyewe yanaathiri tarehe ya mwisho iliyowekwa ya Zuma kujisalimisha.

Mahakama ya Katiba ilisema kwamba ilipokea ombi la kukata rufaa la Bw Zuma Ijumaa na italifanyia maamuzi ya ombi hilo mnamo Julai 12.

Wakati huo huo, Taasisi ya Jacob Zuma, mfuko wa misaada wa rais wa zamani, ilisema rufaa dhidi ya amri ya kukamatwa itasikilizwa na mahakama kuu ya jimbo la KwaZulu-Natal Jumanne.

Zuma na wafuasi wake wanasemaje?

Bwana Zuma anasema hatajisalimisha polisi
Image: EPA

"Hakuna haja ya mimi kwenda jela leo," Bw Zuma aliwaambia wanahabari siku ya Jumapili nje ya makazi yake huko Nkandla katika jimbo la Kwa-Zulu Natal.

Amedai kwamba "amezabwa adhabu ya kwenda jela bila ya kusikilizwa" na kudai kwamba "Afrika Kusini inarejea kwa kasi katika utawala wa kibaguzi."

Mfuasi wake mmoja, Lindokuhle Maphalala, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kama mkuu wa polisi angekuja kumkamata Zuma "kwanza inabidi aanze na sisi."

"Makabiliano mabaya yangetokea kama kama polisi wangejaribu kunikamata," Jacob Zuma aliwaambia mamia ya wafuasi wake ambao walilipuka kwa miluzi na shangwe.

Mkusanyiko huo wa wafuasi wa Zuma ni haramu kwa kuwa unavunja kanuni za kudhibiti ugonjwa wa corona, lakini hakukuwa na askari walioenda kuwaondosha watu. Hali hiyo imewafanya baadhi ya watu kuona kuwa kiongozi huyo yupo juu ya sheria kwa kuwa ana nguvu kubwa ya kisiasa.

Zuma anakabiliwa na kashfa gani?

Jacob Zuma 79 aliondolewa mamlakani mnamo 2018, baada ya miaka tisa madarakani, akikabiliwa na shutuma za ufisadi.

Wafanyabiashara walishutumiwa kwa kula njama na wanasiasa kushawishi mchakato wa kufanya uamuzi.

Lakini Bwana Zuma amerudia kusema kuwa yeye ndiye mwathiriwa wa njama za kisiasa. Amekataa pia kutoa ushirikiano katika uchunguzi juu ya makosa wakati wa uongozi wake.

Rais huyo wa zamani alitoa ushahidi mara moja tu wakati wa uchunguzi wa kile kilichojulikana kama "kutekwa kwa serikali" lakini akakataa kujitokeza tena baadaye.

Katika suala tofauti la kisheria, Bwana Zuma alikana shutuma zilizomkabili katika kesi yake ya ufisadi iliyohusisha makubaliano ya silaha ya thamani ya dola bilioni 5 kutoka miaka ya 1990.

Umati wa wafuasi wamekusanyika nje ya nyumba yake katika mkoa wa KwaZulu-Natal - wengi wakitarajia kuhakikisha kuwa hapelekwi gerezani.

Mvutano wa kisiasa umekuwa ukiongezeka nchini Afrika Kusini wiki hii, huku wanachama wa chama cha maveterani wa jeshi wakitishia kwamba nchi hiyo italegalega ikiwa Bwana Zuma atakamatwa.

Chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC, ambacho Bwana Zuma alikuwa akiongoza, kimetaka utulivu. Lakini akiogopa mgongano mkutano wa kamati yake kuu ya kitaifa umeahirishwa wikiendi hii.

View Comments