In Summary

• Shirika la Nairobi Metropolitan (NMS) limeamrishwa kufunga eneo kutupa taka la Dandora katika muda wa miezi sita ijayo.

• Katika Hukumu iliyotolewa Alhamisi Asubuhi, Jaji Bor aliamuru NMS kuzima jalala hilo ndani ya miezi sita.

• Pia watawasilisha ripoti kortini kila baada ya miezi minne kuonyesha ubora wa maji wa sampuli kutoka maeneo 12 tofauti ambapo mto unapita.

Mkurugenzi wa NMS Meja jenerali Mohamed Badi

Shirika la Nairobi Metropolitan (NMS) limeamrishwa kufunga eneo kutupa taka la Dandora katika muda wa miezi sita ijayo.

Jaji wa mahakama ya Mazingira na Ardhi Kossy Bor ameamuru NMS kufunga eneo hilo na kulibadilisha liwe salama katika kipindi hicho.

Katika kesi iliyowasishwa na Isaya Odando na Wilson Yatta kwa niaba ya Kituo cha Ufanisi huko Korogocho wakilalamika kuwa jalala la Dandora limejazwa na moshi unaotokana na kuchomwa kwa taka za plastiki ambazo hutoa gesi zenye sumu na kemikali zinazo sababisha maradhi ya saratani.

Walikuwa wameshtaki NMS, Nema, waziri wa Mazingira na serikali za Kaunti za Nairobi, Machakos, Kiambu, Kilifi, Makueni na Tana River.

Walishutumu NMS na Nema kwa kukiuka haki zao na wakatafuta maagizo ya kuwalazimisha kuchukua hatua za kukomesha uchafuzi wa mito ya Nairobi na Athi.

Katika Hukumu iliyotolewa Alhamisi Asubuhi, Jaji Bor aliamuru NMS kuzima jalala hilo ndani ya miezi sita.

"Huduma za Metropolitan Nairobi zinaamrishwa kuchukua hatua za kusitisha utupaji taka wa Dandora na kuuhamishia sehemu nyingine ndani ya miezi sita kuanzia tarehe ya uamuzi huu," mahakama iliamuru.

NMS pia imeamriwa kuchukua hatua zote za kiutendaji kuhakikisha kuwa taka kwenye jalala la Dandora zinasimamiwa kwa njia ambayo inalinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari mbaya kutoka kwa taka.

Mahakama

"NMS lazima ihakikishe kwamba hakuna uchomaji wa plastiki au taka nyingine katika jalala la Dandora," mahakama iliagiza.

Korti iliamuru pia watengeneze njia za usimamizi na utupaji salama wa taka kutoka kaunti ya Nairobi kwa njia nzuri ya mazingira kulingana na kanuni za Usimamizi na utunzi wa Mazingira (Udhibiti wa Taka) za 2006.

Shirika hilo pia limeelekezwa kuendeleza mpango na mkakati wa kusafisha Mito ya Nairobi na Athi kwa kufanya usafi wa haraka wa Mto Nairobi kutoka chanzo hadi mto Sabaki huko Malindi hadi mto wote uwe safi bila uchafuzi wa mazingira.

Pia watawasilisha ripoti kortini kila baada ya miezi minne kuonyesha ubora wa maji wa sampuli kutoka maeneo 12 tofauti ambapo mto unapita.

"Ndani ya siku 30 mshtakiwa atabaini kemikali hatari kwa mazingira na afya haswa katika eneo la kutupa taka la Korogocho, Mukuru na Dandora," jaji aliamuru.

Korti iliagiza Nema pia kufanya mipango iliyokusudiwa kuhamasisha umma, kuongeza elimu ya mazingira juu ya uchafuzi wa Mto Nairobi na Athi na kukuza na kusambaza miongozo inayohusiana na kuzuia uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa Mto Nairobi na Athi.

Jaji Bor pia aliwatunuku washtaki fidia ya shilingi 10,000 kila mmoja kama fidia ya madhara yaliyosababishwa na jalala na pia walipewa gharama za kuwasilisha kesi.

View Comments