In Summary

•Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19) ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia wanadaiwa kukamatwa na polisi kutoka kituo cha polisi cha Manyatta mnamo Jumapili.

•Kwa siku tatu walitafutwa kila mahali walikodhaniwa kuwa ikiwemo kwa kituo cha polisi cha Manyatta ila juhudi zote ziliangulia patupu.

•Siku ya Jumatano wazazi hao waliandamana na kikundi kikubwa cha wanakijiji waliokuwa wamejawa na ghadhabu na kushambulia kituo cha polisi cha Manyatta wakidai majibu kuhusiana na kifo cha watoto wao.

Marehemu Benson Njiru na Emmanuel Mutura
Image: HISANI

Wazazi wa  ndugu wawili ambao miili yao ilipatika katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Embu  Level 5 mnamo Jumanne wananyooshea maafisa wa polisi kwa kifo cha watoto wao.

Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19) ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia wanadaiwa kukamatwa na polisi kutoka kituo cha polisi cha Manyatta mnamo Jumapili.

Baada ya kukamatwa kwao haikujulikana walikokuwa  na familia ikaanza juhudi za kuwatafuta.

Kwa siku tatu walitafutwa kila mahali walikodhaniwa kuwa ikiwemo kwa kituo cha polisi cha Manyatta ila juhudi zote ziliangulia patupu.

Familia imesema kuwa walifahamishwa kuwa maafisa kutoka Manyatta walikamata ndugu hao wawili katika soko ya Kianjokoma walikokuwa wanauza nyama ya nguruwe siku ya Jumapili.

Baada ya hapo hawakuonekana tena hadi Jumanne wakati ambapo miili yao ilipatikana katika mochari moja maeneo ya Embu.

Wazazi wa Njiru na Mutura, John Ndwiga na Catherine Wawira wanalaumu maafisa hao kwa kifo cha wanao.

Siku ya Jumatano wazazi hao waliandamana na kikundi kikubwa cha wanakijiji waliokuwa wamejawa na ghadhabu na kushambulia kituo cha polisi cha Manyatta wakidai majibu kuhusiana na kifo cha watoto wao.

"Mbona walisita kutupatia habari kuhusu ajali iliyotokea?" Wazazi waliuliza.

Bi Wawira alidai kuwa maafisa hao walisababisha kifo cha wanawe kwani walishindwa kueleza vizuri kuhusu tukio hilo.

"Aki watoto wangu walikufia mikononi ya serikali. Kwa ni serikali ni ya nini? Ni ya kutusaidia ama ni ya kutuua? Wametuulia watoto kwanini? Kwani wamefanya nini? Kuna kituo cha polisi Githangari, Kwa nini polisi wa Manyatta walikuja Kianjokoma? Kwani watu wa Githangari walikuwa wapi na kuna askari? Sasa tunasema afadhali askari wakae tujisaidie" Wawira aliyekuwa amejawa na hasira ya kupoteza wanawe alisema.

Waandamanaji walifunga mabarabara na kuwasha mioto na kudhalilisha shughuli za biashara wakilalamikia tukio hilo.

Polisi walifika na kujaribu kutuliza hali ila wakajipata pabaya wakati waandamanaji hao walichoma gari lao ambalo walikuwa wanatumia kutuliza maandamano.

View Comments