In Summary

• Juhudi za kutafuta mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka saba aliyetoweka kwa njia za kutatanisha jumapili ya tarehe ishirini na tatu huko Dagoretti kusini zimefikia kikomo kwa njia ya kutamausha baada ya mwili wa mtoto huyo kupatikana ukiwa umetupwa kichakani maeneo ya Kirigu, Alhamisi tarehe 27

Crime scene
Image: HISANI

Juhudi za kutafuta mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka saba aliyetoweka kwa njia za kutatanisha Jumapili ya tarehe ishirini na tatu huko Dagoretti kusini zimefikia kikomo kwa njia ya kutamausha baada ya mwili wa mtoto huyo kupatikana ukiwa umetupwa kichakani maeneo ya Kirigu, Alhamisi tarehe 27.

Makachero wa DCI walioko eneo hilo, kwa uchunguzi wa kindani walimtafuta mtoto huyo baada ya kupokea ripoti iliyorekodiwa na mamake maremu katika kituo cha polisi cha Kirigu, na tayari walikuwa wamemzuilia mshukiwa mmoja kwa jina la Maxwell Muigai, 20, ambaye ni binamuye babake marehemu.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa na DCI, mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni baada ya uchunguzi wa kina kumuonesha kuwa alijaribu kuomba fidia kwa familia ya mtoto huyo ili kumwachilia mwanao.

“Baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa, makachero wa DCI walibaini kuwa jioni hiyo ambayo mtoto huyo alitoweka, Muigai alimuita marehemu  alipokuwa akicheza nje ya nyumba yao, kabla ya kutoweka naye kusikojulikana,” DCI imesema.

Ripoti ya DCI inaelezea Zaidi kwamba ilipofika usiku wa siku hiyo, wazazii wa marehemu waligundua kuwa mwanao harudi kwa nyumba na hapo ndipo walipigwa na pumbuazi kwamba mwanawe ametoweka.

“Baada ya kupata ushahidi huu wote unaoashiria kuwa mtuhumiwa alihusika pakubwa katika kutoweka kwa mtoto huyo, Alhamisi 27 Muigai alishurutishwa kupeleka makachero wa DCI wakishirikiana na polisi kutoka kituo cha Kirigu hadi sehemu aliyotendea ukatili huo kwa mtoto huyo mdogo baada ya familia kukosa kutuma fidia kama alivyoamuru awali kupitia njia ya simu,” DCI iliongeza.

Maafisa wa polisi waliuchukua mwili wa mtoto huyo kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha PCEA Kikuyu, huku uchunguzi wa upasuaji ukisubiriwa kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.

View Comments