In Summary

 

  • Rais Kenyatta aliwatuza maafisa waliofuzu katika nyanja mbali mbali wakiongozwa na Brian Mathinji Ngure ambaye aliibuka afisa bora wa kadet katika uongozi na usimamizi
  • Mika Mohamed Yona wa Tanzania alishinda nafasi ya afisa bora kutoka nchi washirika huku Joekevin Muiga Rugara akiibuka afisa bora zaidi katika masomo ya kawaida.

 

Rais Uhuru Kenyatta

Na   PSCU

 Rais Uhuru Kenyatta ameshauri Jeshi la Ulinzi nchini (KDF) kuekeza zaidi katika mafunzo ili kujiandaa vyema kukabili vitisho vya usalama vinavyoibuka.

Rais ambaye aliandamana na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta, alikariri kwamba mafunzo sharti yaangazie kutoa ujuzi utakaoandaa jeshi kukabiliana na changamoto mbali mbali kutoka nyanja za kawaida na zisizo za kawaida.

“Ili kudhibiti kikamilifu chamngamoto za kiusalama katika karne ya 21, mafunzo katika jeshi sharti yaambatane vyema na vitisho vinavyoibuka katika nyanja zote na majukumu makubwa yanayowekwa kwa mabega ya jeshi letu,” kasema Rais.

Rais Kenyatta alisema hayo Alhamisi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Lanet, Kaunti ya Nakuru, ambako alizindua kundi la nane la maafisa wa Kadet ambalo limepata mafunzo ya miaka mitatu ya Shahada ya Sayansi ya Kijeshi na Usalama.

Maafisa hao wa Kadet, ambao walianza masomo hayo ya shahada inayotolewa na Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa ushirikiano na Wizara ya Ulinzi mnamo mwaka wa 2017, watapewa vyeti vya kuhitimu mwezi ujao.

Rais Uhuru Kenyatta

Akihutubia maafisa hao wanaofuzu, Rais Kenyatta alisema wanafaa kutumia ujuzi, utaalamu na uwezo waliopata  kuhudumia na kulinda uhuru wa taifa, raia wake na kanda.

“Ni muhimu kusisitiza kwamba kusoma ili kujipatia ujuzi na kuboresha ujuzi na uwezo wako kutakuwa juhudi za kila siku katika muda wote wa kazi yako ya kijeshi,” kasema Rais Kenyatta.

Alipongeza maafisa hao wapya na akawashauri wahakikishe kwamba kujitolea kwao katika maadili ya bidii, umakini na ufanisi hakutapungua kamwe siku zote za kazi yao.

“Tunatarajia mengi kutoka kwenu, lakini matarajio yetu hayapiti uwezo wenu wa kuyatimiza; vile vile tunawahimiza siku zote muishi kuambatana na kanuni za Kiapo cha Maafisa na msiruhusu kamwe viwango vya juu vya utaalamu, ujasiri na kujitolea kwa kazi ambavyo vimewekwa na waliowatangulia kupungua hata kidogo," kasema Rais.

Akisema maafisa waliofuzu wanajumuisha wengine kutoka Rwanda, Tanzania na Uganda, Rais Kenyatta alisema mafunzo hayo ya kiwango cha juu waliyopata kutoka chuo hicho cha jeshi yanafaa kuimarisha ushirikiano wa kiusalama katika kanda.

“Muhimu zaidi, nina imani kwamba urafiki ulioanzishwa hapa miongoni mwenu utachangia kuimarisha uhusiano wetu wa kitaifa na harakati zetu za pamoja za kukabili changamoto za kiusalama tunazoendelea kupata katika kanda yetu,” kasema Rais.

Rais Kenyatta aliwatuza maafisa waliofuzu katika nyanja mbali mbali wakiongozwa na Brian Mathinji Ngure ambaye aliibuka afisa bora wa kadet katika uongozi na usimamizi, akishinda tuzo la Upanga wa Heshima akifuatwa na Safia Diramu Dida aliyechukua nafasi ya pili.

Denis Melita Nanyukoko alishinda tuzo la afisa wa Kadet masomo ya kitaalamu huku David Paul Gitonga akinyakua nafasi ya pili katika kitengo hicho.

Tuzo la afisa bora zaidi wa Cadet katika masuala ya tabia lilinyakuliwa na Paul Odhiambo Olwal huku nafasi ya pili ikitwaliwa na Endrico Lopua Elimlim.

Mika Mohamed Yona wa Tanzania alishinda nafasi ya afisa bora kutoka nchi washirika huku Joekevin Muiga Rugara akiibuka afisa bora zaidi katika masomo ya kawaida.

Gwaride hilo la uzinduzi ilihudhuriwa na Gavana wa Kaunti ya Nakuru Lee Kinyanjui, Waziri wa Ulinzi Monica Juma Mkuu wa Majeshi Jemedari Robert Kibochi. 

Wengine waliokuwepo ni Inspekta Mkuu wa Polisi Hilary Mutyambai na Kamanda wa chuo hicho Meja Jenerali Peter Njiru kati ya viongozi wengine wa kitaifa na kijeshi.

  

View Comments