Video inayoenezwa mitandaoni ikionyesha afisa wa polisi akiibiwa simu na mtu aliyeabiri pikipiki ni ghushi, huduma ya polisi nchini Kenya(NPS) imedhihirisha.
Video ambayo ilisambazwa sana mitandaoni siku ya Jumatano ilionyesha alionekana kuwa afisa wa polisi akizungumza kwa simu akiwa amesimama kwenye barabara iliyo katika mzunguko wa Roysambu.
Afisa huyo anapoendelea kupiga simu, pikipiki iliyokuwa imebeba abiria wawili ilionekana kupita mbele yake na abiria aliyekuwa amekaa nyuma alionekana kunyakua simu ambayo afisa huyo alikuwa ameshika kwenye masikio.
Video hiyo ilisisimua wanamitandao wengi ambao waliisambaza kabisa kweli na kuibua gumzo kote nchini.
Hata hivyo, NPS inayoongozwa na Inspekta Jenerali Hilary Mutyambai wamejitokeza kupinga uhalali wa tukio hilo.
Kulingana na ujumbe uliochapishwa kwenye akaunti rasmi ya NPS katika mtandao wa Twitter mida ya saa nne kasorobo usiku wa Jumatano, upelelezi ulibaini kuwa tukio hilo halikutendeka na video hiyo ilikuwa imetengenezwa kwa kompyuta.
"Upelelezi wetu umeonyesha kuwa video ambayo inaenea mitandaoni ikionyesha afisa wa polisi akipokonywa simu ni ghushi na ina malengo mabaya. Tunasihi umma kuipuuzilia mbali" NPS waliandika.