In Summary

•Haijathibitishwa wazi kile ambacho vijana hao walikuwa wameenda kufanya pale ila mpango wao uligonga mwamba baada ya baadhi ya wasichana kuwaona na kupiga nduru mara moja.

•Mvulana ambaye aliachwa nyuma alikamatwa na kupewa kichapo cha mbwa ambacho kilimuacha  katika hali mahututi.

crime scene 1

Mwanafunzi mmoja wa kidato cha nne kutoka shule ya upili ya wavulana ya Gathiruini, kaunti ya Kiambu alifariki baada ya kupigwa kitutu na wasichana kutoka shule jirani ya wasichana.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 kwa ushirikiano na wenzake wengine watano walikuwa wametoroka kutoka shule yao mida ya saa kumi asubuhi ya kuamkia Alhamisi na wakafululiza hadi shule ya upili ya wasichana ya Komothai iliyo umbali mfupi kutoka shule yao.

Kulingana na DCI, sita hao walipofanikiwa kuingia ndani ya shule hiyo ya wasichana walinyemelea hadi kwenye bweni  la Phoeb.

Haijathibitishwa wazi kile ambacho vijana hao walikuwa wameenda kufanya pale ila mpango wao uligonga mwamba baada ya baadhi ya wasichana kuwaona na kupiga nduru mara moja.

Wanafunzi wengine pamoja na walimu na walinzi walikimbia pale kujionea kilichokuwa kinaendelea ila wavulana watano kati ya sita waliokuwa wameingia kwenye bweni ya wasichana kwa njia haramu  wakaweza kutoroka na kurudi kwa shule yao huku wakiacha mwenzao mmoja nyuma.

Mvulana ambaye aliachwa nyuma alikamatwa na kupewa kichapo cha mbwa ambacho kilimuacha  katika hali mahututi.

Baada ya hayo alikimbizwa katika hospitali ya Kigumo ambako alifariki kutokana na majeraha mabaya mwilini alipokuwa anahudumiwa.

Wapelelezi walifika kwenye eneo la tukio na kupata miti inayoaminika kutumika kushambulia marehemu. 

Maafisa wa DCI hata hivyo wametoa onyo kali kwa umma dhidi ya kuchukua sheria mikononi na kuwaruhusu washukiwa wajibu mashtaka dhidi yao mahakamani.

View Comments