In Summary

•Sifuna ameomba wananchi wasichukulie matamshi ya Junet kwa uzito huku akieleza kwamba mwanasiasa huyo alikuwa anafanya mzaha tu.

•Amehakikishia wananchi kwamba serikali ambayo Raila Odinga ataunda haitabagua watu kutoka maeneo yoyote na itahusisha Wakenya wote.

•Wanasiasa mbalimbali haswa kutoka eneo la mlima Kenya na bonde la ufa ikiwemo Kimani Ichungwa, Moses Kuria, Caleb Koistany na Isaac Mwaura wameeleza kutoridhishwa kwao na matamshi hayo ya Junet.

b6251efb2cdb00bc

Huku mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed akiendelea kukosolewa sana kufuatia matamshi yake kuwa serikali itakuwa ya wazaliwa wa Nyanza iwapo Raila Odinga atanyakua ushindi kwenye chaguzi za mwaka ujao, katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna amejitokeza kumtetea kiranja huyo wa walio wachache bungeni.

Sifuna ameomba wananchi wasichukulie matamshi ya Junet kwa uzito huku akieleza kwamba mwanasiasa huyo alikuwa anafanya mzaha tu.

Kulingana na Sifuna, mbunge huyo wa Suna anaelewa kwamba iwapo kinara wa ODM atashinda kiti cha urais serikali yake itahusisha kila Mkenya wala sio watu kutoka eneo moja kama alivyosema siku ya Ijumaa akiwa Nyamira.

"Junet alisema kitu kwa utani lakini kuna watu kumbe hawajui utani. Wamekasirika sana. Mimi nawaambia Junet Mohammed tumetembea na yeye Kenya yote. Tulienda na yeye Sipiri, tulienda naye eneo la Magharibi na anajua watu wa magharibi watakuwa kwa serikali ya Odinga, tulienda naye upande wa North Eastern na Baba ndiye mgombeaji wao. Kwa hivyo msichukue kitu ambacho mtu amesema kwa mzaha muanze kuleta makasiriko" Sifuna alisema.

Sifuna alihakikishia wananchi kwamba serikali ambayo Raila Odinga ataunda haitabagua watu kutoka maeneo yoyote na itahusisha Wakenya wote.

"Serikali ya Raila Amollo Odinga si serikali ya watu wa Nyanza, ni serikali ya nchi nzima kwa sababu baba anasimama kwa msingi wa azimio la umoja" Alisema Sifuna.

Siku ya Ijumaa Junet alipokuwa anatoa hotuba yake kwenye hafla ya kuchanga ambayo ilikuwa imehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwemo Raila Odinga, waziri Fred Matiang'i na Mutahi Kagwe, alisikika akihakikishia wakazi kwamba uongozi utakuwa wao iwapo kinara wa ODM atachukua usukani kutoka kwa rais Uhuru Kenyatta.

Junet alimuomba waziri wa afya Mutahi Kagwe  asikasirishwe na matamshi yake huku akidai kwamba eneo alilotoka la Mlima Kenya limekuwa likitawala kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini.

"Hapa Nyanza sisi ni watu moja, sisi ni jamii moja. Tusiwe na wasiwasi. Baba akishinda, serikali ni yetu watu wa Nyanza, Sitaki watu wa gazeti wasikie hiyo, Mutahi Kagwe anaweza kasirika, lakini ata nyinyi mlikuwa nayo miaka ishirini na kadharika. Safari hii ni yetu watu wa Nyanza. Mutahi utakuja hapa kama mgeni" Junet alisema.

Matamshi ya mwanasiasa huyo hata hivyo hayajapokewa vyema haswa na wafuasi wa mpinzani mkubwa wa Raila Odinga, naibu rais William Ruto.

Wanasiasa mbalimbali haswa kutoka eneo la mlima Kenya na bonde la ufa ikiwemo Kimani Ichungwa, Moses Kuria, Caleb Koistany na Isaac Mwaura wameeleza kutoridhishwa kwao na matamshi hayo ya Junet.

View Comments