In Summary

• Kinara wa walio wachache Peter Imwatok aliwasilisha hoja hiyo, akisema viongozi wanaostahili wanapaswa kutambuliwa wakiwa hai, sio wanapofariki.

• Alisema Raila, amestawisha pakubwa maendeleo ya kidemokrasia na kiuchumi nchini Kenya.

• Hii ni barabara ya nne kubadilishwa jina mwaka huu katika kaunti ya Nairobi.

Barabara ya Mbagathi imebadilishwa jina na sasa itajulikana kama Raila Odinga Way baada ya bunge la kaunti ya Nairobi kupitisha hoja ya kubadilisha jina la barabara hiyo.

Barabara hiyo ilipewa jina la kiongozi wa chama cha ODM Alhamisi usiku.

Katika bango hilo, kulikuwa na pande mbili moja iliyoandikwa barabara ya Langata na nyingine ya Raila Odinga inayoonyesha Njia ya Mbagathi.

Hii ni barabara ya nne kubadilishwa jina mwaka huu katika kaunti ya Nairobi.

Kinara wa walio wachache Peter Imwatok aliwasilisha hoja hiyo, akisema viongozi wanaostahili wanapaswa kutambuliwa wakiwa hai, sio wanapofariki.

Alisema Raila, mgombea urais, ameboresha pakubwa maendeleo ya kidemokrasia na kiuchumi nchini Kenya.

Hata hivyo, Nairobi haina sera ya kutaja mitaa, barabara au majengo.

Mwezi Machi, barabara ya Eastleigh First Avenue ilibadilishwa jina na kuitwa Mohammed Yusuf Haji Avenue kwa heshima ya seneta wa Garissa aliyefariki Februari.

Barabara ya Kapiti Crescent mtaani South B ilibadilishwa jina na kuitwa jina la gwiji wa soka nchini marehemu Joe Kadenge na Accra road kubadilishwa jina na kuitwa aliyekuwa kiongozi wa chama cha Ford Asili Kenneth Matiba (aliyefariki).

Mwezi Mei, Naibu Gavana wa Nairobi Ann Kananu alibadilisha jina la Barabara ya Dik Dik huko Kileleshwa hadi jina la Francis Atwoli, katibu mkuu wa COTU.

View Comments