In Summary

• Mwathiriwa alivamiwa karibu na Cabanas baada ya kuteremka kutoka kwa matatu ambayo alichukua kutoka eneo la Donholm ambapo alikuwa ametoa pesa za mradi fulani.

• Hili ni tukio la nne kutokea katika kipindi cha wiki mbili ambapo watu wanaotoa pesa benki wamevamiwa na kuibiwa.  

• Alipigwa risasi ya pajani alipojaribu kupingana na majambazi hao waliokuwa kwenye pikipiki.

Lori lashika moto baada ya ajali ya barabarani iliyohusisha magari manne katika eneo la Maltauro kaunti ya Narok Jumamosi jioni.
Image: KIPLAGAT KIRUI

Polisi wanasaka genge lililompiga risasi na kumjeruhi vibaya mwanamume mmoja kabla ya kumpora Shilingi milioni 1.1 muda mfupi baada ya kuzitoa kwenye benki eneo la Embakasi, Nairobi. 

Mwathiriwa alivamiwa karibu na Cabanas baada ya kuteremka kutoka kwa matatu ambayo alichukua kutoka eneo la Donholm ambapo alikuwa ametoa pesa za mradi fulani.  

Polisi wanasema wanashuku kuwa alifuatwa na genge lililokuwa likifahamu shughuli zake katika benki hiyo kabla ya ufyatuaji risasi na wizi kutokea.

Alipigwa risasi ya pajani alipojaribu kupingana na majambazi hao waliokuwa kwenye pikipiki.  Genge hilo lilitoroka na pesa huku mwathiriwa akikimbizwa hospitalini ambako amelazwa.

Hili ni tukio la nne kutokea katika kipindi cha wiki mbili ambapo watu wanaotoa pesa benki wamevamiwa na kuibiwa.  

Polisi wamewaonya wale wanaonuia kutoa kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa benki kuwa makini na kuchukuwa tahadhari za kiusalama kutokana na kuwepo kwa genge linalowaandama watu baada ya kutoa pesa.

Kwingineko, 

Mwanamume mmoja aliteketea hadi kufa Jumatano usiku katika kisa cha moto mtaani Mukuru eneo la Lungalunga, Nairobi.

Mwathiriwa alikuwa amelala moto ulipozuka na kuteketeza majengo kadhaa katika kitongoji hicho cha mabanda.

Kisa hiki kiliwaacha watu wengi bila makao. Polisi wanasema watu wengine sita walipata majeraha madogo walipokuwa wakijaribu kudhibiti moto huo ili usienee kwa nyumba zingine.

Chanzo cha moto huo bado hakijabainika lakini wataalamu wanachunguza. Mwili wa mwenda zake ulihamishwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Kulingana na polisi visa vingi vya moto katika mitaa ya mabanda vinatokana na uunganisho haramu wa umeme

View Comments