In Summary

•Wahasiriwa walikuwa wanaelekea upande wa Nuu kuhudhuria harusi ya ndugu ya Padre Benson Kityambu wa kanisa la katoliki la Mwingi.

•Ndugu wawili wa kidini ambao walikuwa wanafanya kazi katika seminari pia walipoteza maisha yao kwenye ajali hiyo.

•Kufikia kusimamishwa kwa shughuli ya uokoaji jioni ya Jumamosi, watu 24 walithibitishwa kufariki huku wengine 12 wakiokolewa.

Wakazi wakitazama maji baada ya basi hilo kuzama
Image: LINAH MUSANGI

Kati ya watu 24 ambao wameripotiwa kufariki kufuatia ajali mbaya ya basi iliyotokea katika mto wa Enziu,eneo la Mwingi  siku ya Jumamosi, 22  walikuwa waumini katika kanisa la St. James Good Shepherd Catholic Church.

Ujumbe wa mawasiliano uliotumwa kwa wanachama wa kanisa hilo ambao umeonwa na Radio Jambo unasema wahasiriwa walikuwa wanaelekea upande wa Nuu kuhudhuria harusi ya ndugu ya Padre Benson Kityambu wa kanisa la katoliki la Mwingi.

Padre Kityambu anaripotiwa kupoteza wapwa wake 11 katika ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa saba alasiri.

Ndugu wawili wa kidini ambao walikuwa wanafanya kazi katika seminari pia walipoteza maisha yao kwenye ajali hiyo.

"Wapendwa waumini na marafiki wa St.James, habari za jioni? Niruhusu niwataarifu kwamba kwaya yetu ya Kanisa Katoliki ya Good Shepherd-Mwingi leo walipata ajali mbaya ya barabarani wakielekea kuhudhuria harusi ya kakake Fr Benson Kityambu huko Nuu.

Dereva alipokuwa akijaribu kuvuka mto Enziu, basi la ST.Josephs Seminary lilipoteza mwelekeo na kusombwa na nguvu za maji. Mpaka sasa tumepoteza wanachama 22. Milli ingine  bado inatafutwa. Wengine wameokolewa na kukimbizwa hospitali ya Mwingi level 4. Padre Kityambu amepoteza wapwa 11.

Pia tumepoteza ndugu wawili wa kidini wanaofanya kazi katika seminari. Wapendwa tuendelee kuombea mahali pema peponi roho za marehemu"  Ujumbe ulisoma.

Kufikia kusimamishwa kwa shughuli ya uokoaji jioni ya Jumamosi, watu 24 walithibitishwa kufariki huku wengine 12 wakiokolewa.

Wanne kati ya 12 waliookolewa ni watoto huku wengine 8 wakiwa watu wazima. 15 kati ya waliopoteza maisha ni kutoka familia moja.

Harusi ambayo ilikuwa ifanyike eneo la Nuu haikuendelea kufuatia msiba huo .

Timu ya waokoaji kutoka Kenya Navy inasaidia katika usakaji shughuli ya uokoaji.

Rais Uhuru Kenyatta, naibu rais William Ruto, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na viongozi wengine wengi wameomboleza walioangamia na kufariji  familia zilizopoteza wapendwa wao.

View Comments