In Summary

•Miili hiyo ilipatikana ikiwa imewekwa kwenye magunia, baadhi ikiwa imefungwa kwa kamba huku ingine ikiwa imeharibika.

•HAKI Africa ilimwandikia DPP Noordin Haji ikiomba kuingilia kati katika kisa cha miili iliyokuwa imetupwa ndani ya Mto Yala.

Mto Yala
Image: MAKTABA

Timu maalum ya uchunguzi imetumwa katika mto Yala ili  kufanyia uchunguzi miili 19 ya watu wasiotambulika ambayo haijadaiwa nayeyote

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa wanahabari siku ya Jumatano, msemaji wa Polisi Bruno Shioso amesema miili hiyo imekuwa pale mtoni kwa muda wa miaka miwili iliyopita..

Miili hiyo ilipatikana ikiwa imewekwa kwenye magunia, baadhi ikiwa imefungwa kwa kamba huku ingine ikiwa imeharibika.

Shioso alitupilia mbali madai kuwa miili hiyo 19 ilitupwa mara moja.

“Licha ya wito wa polisi, hakuna aliyejitokeza kudai miili hiyo,” Shioso alisema.

Shioso ametoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zaidi kuhusu miili hiyo  kujitokeza ili  kusaidia katika uchunguzi huo.

HAKI Africa ilimwandikia DPP Noordin Haji ikiomba kuingilia kati katika kisa cha miili iliyokuwa imetupwa ndani ya Mto Yala.

Kumekuwa na mjadala mkubwa miongoni mwa Wakenya kuhusu miili 19 ambayo ilioopolewa mtoni huo.

Baadhi ya Wakenya walijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kueleza wasiwasi wao kuhusu ripoti hizo, huku wakimuomba Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kufungua uchunguzi kuhusu kisa hicho.

Ripoti hiyo kuhusu Mto Yala ilipeperushwa kwa mara ya kwanza na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu waliotembelea eneo ambalo miili hiyo inasemekana kupatikana.

Mnamo Oktoba 20, 2021, chumba cha kuhifadhi maiti cha Yala kilizika miili tisa ambayo haikutambuliwa ili kuunda nafasi katika chumba cha kuhifadhi maiti. Maafisa walisema hospitali hiyo imekuwa ikipokea miili kutoka mtoni.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Gem, Charles Chacha alisema wameanza uchunguzi wao baada ya wakaazi wa Yala kutoa wasiwasi kuhusu miili hiyo.

View Comments