In Summary

• Afisa Mkuu Mtendaji Tabitha Karanja amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati akisema juhudi za kufanya majadiliano na kamishna Mkuu wa KRA zimegonga mwamba.

• Kiwanda cha kutengeneza bia kimekuwa katika vita vya muda mrefu vya ushuru huku KRA ikiitaka  kampuni hiyo kufunga mara kadhaa.

• "Juhudi za kujadili upya mkataba na Kamishna wa Idara ya Ushuru wa Ndani ya KRA na kupata stempu za mapato hazikufaulu." Alisema.

Mwenyekiti wa kampuni ya Keroche ya kutengeneza pombe Tabitha Karanja

Makumi ya wafanyikazi wanatazamiwa kupoteza kazi katika kampuni ya Keroche Breweries kufuatia uamuzi wa Mamlaka ya Ushuru ya Kenya kuifunga kampuni hiyo kutokana na malimbikizo ya ushuru ya Sh332 milioni.

Kuzimwa huko kunajiri hata baada ya kampuni hiyo yenye makao yake mjini Naivasha kuomba muda zaidi kutoka kwa KRA kulipa malimbikizi ya ushuru, akisema janga la Covid-19 limeathiri vibaya mtiririko wa mapato yake.

Afisa Mkuu Mtendaji Tabitha Karanja amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati akisema juhudi za kufanya majadiliano na kamishna Mkuu wa KRA zimegonga mwamba.

"Tuna uhakika kwamba suala hili linaweza kutatuliwa kwa amani kwani tuko tayari kulipa ushuru unaohitajika ikiwa KRA itafungua kiwanda chetu cha kutengeneza bia," Karanja alisema.

Kiwanda hicho cha kutengeneza bia kimekuwa katika vita vya muda mrefu vya ushuru huku KRA ikilazimisha kampuni hiyo kufunga mara kadhaa.

Karanja, ambaye alihutubia wanahabari siku ya Ijumaa akiwa ameandamana na wafanyikazi, aliapa kuwa atapambana kunusuru kiwanda hicho, akibainisha kuwa katika kilele cha shughuli zake, kampuni hiyo ilikuwa ikituma zaidi ya Shilingi milioni 200 kwa serikali kila mwezi.

Alisema malimbikizi ya ushuru ya Shilingi milioni 332, ambayo ni chanzo cha mzozo wa sasa, yaliongezeka kutoka Februari 2021 ambayo kampuni hiyo iliafikia  makubaliano na KRA kuhusu jinsi ya kuirejesha.

"Hata hivyo mnamo Desemba 2021, KRA ilifunga kiwanda na kutoa notisi za wakala kwa benki 36 na hatukuweza kuzalisha au kupata fedha za kusaidia katika kulipa madeni," Karanja alisema.

"Juhudi za kujadili upya mkataba na Kamishna wa Idara ya Ushuru wa Ndani ya KRA na kupata stempu za mapato hazikufaulu." Alisema.

Karanja alifichua kuwa mamlaka hiyo ilifunga kiwanda hicho huku zaidi ya lita milioni mbili za bia zenye thamani ya shilingi milioni 512 zikiwa bado ziko kwenye matangi. Alisema pombe hiyo itaharibika katika muda wa siku saba. 

"Hii imemaliza rasilimali zetu zote na kwa bahati mbaya ikiwa hakuna kitakachofanyika katika siku saba zijazo, tutalazimika kumaliza bia yote na kuachisha kazi zaidi ya wafanyikazi 250 wa moja kwa moja," alisema. 

Katika ombi lake kwa Rais, Karanja aliomba kufunguliwa kwa kiwanda hicho na KRA kuwapa muda wa nyongeza wa miezi kumi na miwili ili kulipa malimbikizo ya ushuru. 

"Keroche ina uwezo wa kutuma zaidi ya Shilingi bilioni 21 kila mwaka za ushuru na kuzingatia vyema rufaa hii kutakuwa ushindi kwa kampuni na KRA."

View Comments