In Summary

•James Maina Kibe alitozwa faini ya shilingi 70,000 baada ya kukubali mashtaka ya kuendesha gari vibaya.

•Baada ya wawili hao kushiriki mazungumzo na kuelewana waliandamana hadi kituo cha polisi na kuandikisha taarifa kuhusu yaliyojiri.

Image: SCREENSHOT

Dereva wa Probox aliyerekodiwa akihatarisha maisha ya mwanadada katika barabara ya Thika Super Highway alishtakiwa katika mahakama ya Milimani siku ya Jumatatu.

James Maina Kibe alitozwa faini ya shilingi 70,000 baada ya kukubali mashtaka ya kuendesha gari vibaya. Leseni yake ya kuendesha gari pia ilisitishwa.

Video ambayo ilienezwa sana mitandaoni ilinasa mwanamke akipiga kelele ndani ya aina ya Probox, nambari ya usajili KBJ 835Z iliyokuwa ikiendeshwa kwa kasi katika  barabara ya Thika.

Maelezo ya video hiyo yalidai kwamba mwanamke huyo ambaye hakutambulishwa alichukuliwa kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta na kuwekwa kwenye Probox kabla ya kung'oa nanga na kutowela kwa mwendo wa kasi.

Juhudi za kulisimamisha gari hilo hazikufua dafu kwani dereva aliondoka kwa kasi. Lakini katika taarifa siku ya Jumatatu, polisi walisema kuwa mwanamke huyo hakutekwa nyara.

Polisi walisema tukio hilo lilihusisha wapenzi wawili ambao walitofautiana baada ya kutoka katika eneo la burudani.

Iliripotiwa kwamba mwadada huyo alitaka kushuka kutoka kwa gari ila mpenziwe alitaka waende naye kwake.

Baada ya wawili hao kushiriki mazungumzo na kuelewana waliandamana hadi kituo cha polisi na kuandikisha taarifa kuhusu yaliyojiri.

View Comments