Naibu Rais William Ruto amesema kuporomoka kwa kwa mchakato wa BBI kumeashiria mwisho wa utapeli wa kisiasa nchini Kenya.
Alisema uamuzi wa Mahakama ya Juu ni ushindi kwa mamilioni ya Wakenya wanaotatizika kujikimu kimaisha.
Alitaja mipango ya kurekebisha katiba kama ulaghai unaolenga kukidhi maslahi ya ubinafsi wa watu wachache.
"Mwisho wa reggae ni mwisho wa utapeli wa kisiasa nchini Kenya," alisema Ruto.
Alibainisha kuwa uamuzi wa Mahakama ya Juu ulikuwa uthibitisho kwamba BBI ilikuwa kinyume cha sheria na ni zoezi lililokiuka katiba.
Alifafanua zaidi kwamba nchi imepoteza miaka minne ya thamani katika zoezi lisilofaa ambalo lilivuruga kutekelezwa kwa Ajenda Nne Kuu zan serikali.
"Ndugu wa Handshake na waendelezaji wa BBI lazima sasa waombe msamaha kwa Wakenya."
Dkt Ruto alikuwa akizungumza siku ya Alhamisi katika Kaunti za Wajir na Lamu ambako alifanya misururu ya mikutano ya hadhara kupigia debe muungano wa Kenya Kwanza.
Ruto alieleza kuwa Wakenya hawakuwa wajinga kutumiwa vibaya na walio mamlakani.
“Vitisho, vitisho na ushawishi haviwezi kubadilisha nchi. Ni wakati wa viongozi kushindana kwenye jukwaa la masuala na sera,” alisema Naibu Rais.