In Summary

•Denis Karani Gachoki anashukiwa kuwa ndiye aliyempiga risasi Muvota mchana peupe siku ya Jumatatu.

•Wawili hao wanadaiwa kozazana kuhusu wanawake ambao wamekuwa wakishiriki mapenzi nao kabla ya kuwaajiri kwenye genge lao.

Denis Karani Gachoki na marehemu Samuel Mugoh Muvota
Image: TWITTER// DCI

Wapelelezi jijini Nairobi wanamsaka jamaa anayeminika kumpiga risasi Samuel Mugoh Muvota katika mtaa wa Mirema, eneo la Kasarani, kaunti ya Nairobi.

Denis Karani Gachoki anashukiwa kuwa ndiye aliyempiga risasi Muvota mchana peupe siku ya Jumatatu.

Mshukiwa anaripotiwa kuwa mfanyikazi wa  Muvota na inadaiwa hivi majuzi walikosana kuhusu mgao wa faida ya biashara yao ya 'Mchele'. Wawili hao pia wanadaiwa kozazana kuhusu wanawake ambao wamekuwa wakishiriki mapenzi nao kabla ya kuwaajiri kwenye genge lao.

Ugomvi huo unaripotiwa kuwa miongoni mwa sababu zilizompelekea Karani kumuua Muvota kwa kumpiga risasi sita.

Karani anaripotiwa kuwa na bunduki ambayo iliibiwa kutoka kwa afisa wa polisi aliyewekewa dawa za kupoteza fahamu katika kilabu kimoja jijini Mombasa mwezi Novemba 2020.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa juhudi za kumkamata Karani zimekuwa zikiangulia patupu kwa kuwa kuna baadhi ya polisi ambao alikuwa amelipa kumuibia siri kila operesheni ya kumkamata inapoanzishwa.

Wapelelezi wa DCI wanashuku huenda Karani tayari amevuka mpaka na kuingia nchini jirani baada ya kutekeleza mauaji Jumatatu. Uchunguzi umebaini kuwa masaa machache baada ya mauaji hayo Karani alikuwa ndani ya msitu wa Burnt Forest.

Yeyote anayefahamu kuhusu alipo mshukiwa amewatakiwa kutoa taarifa  kupitia nambari ya bure 0800 722 203.

Muvota aliuawa Jumatatu katika eneo la Mirema dakika chache baada ya kuchukua mtoto anayeamika kuwa bintiye shuleni.

Marehemu anaripotiwa kuwa na wake saba ambao wote waliishi maisha ya kifahari.

View Comments