In Summary

Kitengo cha DCI kilitoa taarifa kwamba kuanzia Jumapili hii wataanza mfululizo wa kuelezea matukio ya uhalifu kupitia picha.

Hii itakuwa njia moja ya kuelimisha, kufahamisha na kuburudisha umma na pia wakinuia kuboresha uhusiano zaidi baina ya umma na kitengo hicho.

Kielelezo
Image: DCI(Facebook)

Kitengo cha polisi wapelelezi wa makosa ya jinai na visa vya wizi na uhalifu wa kimabavu, DCI kimetoa taarifa kwamba kuanzia Jumapili hii wataukuwa wanaonesha vilelezo vya baadhi ya sehemu na visa vya uhalifu kama njia moja ya kuelimisha, kufahamisha na kuburudisha umma.

Katika taarifa ambayo ilichapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa DCI, walisema kwamba zoezi hilo linalenga kuboresha uhusiano kati ya umma na na wapelelezi hao ili kupatia kitengo hicho sura ya kibinadamu na kuifanya kuwa rahisi kwa umma kutowaogopa bali kuripoti kitendo chochote cha uhalifu kinachotokea karibu nao.

Wakitolea mfano wa polisi mmoja wa kitengo cha GSU ambaye mazoezi yake ya kijeshi yalimsaidia kuwapiku wahalifu ambao walimvamia alipokuwa akirejea kambini katika eneo la Mihang’o mtaani Kayole, polisi huyo alikuwa na wanawake wawili ambao baada ya kuvamiwa walichana mbuga na kumuacha mpambanaji wao baina ya genge la majambazi.

Katika kisa hicho ambacho DCI walikiripoti wiki kadhaa zilizopita walisema mazoezi murua ya kijeshi ndiyo yalimsaidia polisi huyo kupambana na majambazi hao ambao baada ya kumpiga mmoja mwingine alichomoa kisu na kumdunga ubavuni kabla ya kuchechemea kuelekea kambini kuwaita wenzake.

Waliporejea katika sehemu ya tukio walipata wezi wale wameondoka ila walifanikiwa kupata meno mawili ambayo yalikuwa ni ya mwizi mmoja ambaye polisi huyo alipiga zito kimo cha nungunungu aliyekomaa.

Visa kama hivi ndivyo vimeleta msukumo kwa kitengo hicho chenye ufuasi mkubwa mitandaoni kuwatangazia wananchi kwamba watandaa vielelezo vya kuonesha baadhi ya matukio ambayo watayachagua, matukio ambayo aghalabu hutokea katika sehemu nyingi tu humu nchini yakiwahusisha wahalifu na wezi wa kimabavu.

Kitengo cha DCI kina ufuasi mkubwa mitandaoni kutokana na uelendi wa ulumbi wao katika kuhadithia matukio mbalimbali yanayotokea nchini, huku wakielezea kwa njia ya ucheshi inayonuiwa kujenga taswira kamili kwa msomaji, jambo ambalo limefanya watu wengi kutaka kusoma simulizi hizo zao pindi wanapozipakia kwani zina ucheshi wa aina yake, kando na kutaarifu kuhusu matukio ya kuhuzunisha kama ubakaji na wizi wa kimabavu.

View Comments