In Summary

•Kufungwa kwa expressway kunafuatia mwisho wa kipindi cha majaribio ambacho madereva walikuwa wamepatiwa.

•Awamu ya majaribio ilikuwa ni kutathmini mradi na kujua nini kifanyike ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi.

Barabara kuu ya Expressway jijini Nairobi, Kenya
Image: The Star//Maktaba

Barabara ya Nairobi Expressway ilifungwa kwa waendesha magari kuanzia Jumamosi, Julai 30 mwendo wa saa tatu usiku.

Kampuni ya Moja Expressway inayosimamia barabara hiyo, ilisema hatua hiyo inafuatia mwisho wa kipindi cha majaribio ambacho walikuwa wamepatia madereva. 

Barabara hiyo inayounganisha upande wa Magharibi wa Nairobi na ule wa Mashariki itaanza kutumika tena mara tu itakapozinduliwa rasmi.

Kampuni hiyo ilisema madereva wataarifiwa na kushauriwa mara huduma zitakaporejea.

"Kipindi cha majaribio kwa Barabara ya Nairobi Expressway, kilichoanza Mei 14, 2022, kimefikia kikomo," Kampuni ya Moja Expressway ilisema katika taarifa.

"Barabara hiyo sasa itafungwa rasmi kuanzia saa tatu usiku Jumamosi, Julai 30, 2022 hadi itakapoanza kutumika rasmi. Kampuni ya Moja Expressway inasikitika kwa usumbufu uliojitokeza na madereva wa magari watapewa ushauri pindi watakaporejesha huduma kwenye barabara hiyo."

Awamu ya majaribio ilikuwa ni kutathmini mradi na kujua nini kifanyike ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa ufanisi.

Katika awamu za majaribio, ajali kadhaa zimeripotiwa katika barabara hiyo, hasa katika kituo cha kulipia ada cha Mlolongo.

Matukio kama haya sasa yanaipa kampuni fursa ya kubuni njia za kuhakikisha kuwa barabara ni salama na madereva wa magari hufuata taratibu za kawaida za uendeshaji ili kuepusha visa vya kutisha.

View Comments