In Summary

• Kama ilivyokuwa wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCPE, Waziri hatarajiwi kutaja majina ya wanafunzi au shule bora.

Watahiniwa wakifanya mtihani wa kitaifa
Image: MAKTABA

Matokeo ya mtihani wa KCSE wa 2022 yanatolewa leo Ijumaa kabla ya kuanza kwa muhula wa kwanza Jumatatu, Januari 23.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alidokeza wakati akitoa matokeo ya KCPE mnamo Desemba 21 kwamba matokeo ya KCSE yangetoka kabla ya shule kufunguliwa.

Waziri anatarajiwa kutoa tangazo hilo katika afisi za Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC).

Kama ilivyokuwa wakati wa kutolewa kwa matokeo ya KCPE, Waziri hatarajiwi kutaja majina ya wanafunzi au shule bora.

Hii ni kwa kuzingatia sera mpya ya serikali ya kusitisha ushindani usio na maana kati ya shule na watahiniwa.

Hapo awali, serikali iliondoa sera ya kurodhesha shule kwa misingi ya matokeo lakini iliendelea kutangaza orodha ya wanafunzi bora.

Katika matokeo ya mtihani wa 2021, Shule ya Upili ya Kenya High iliibuka bora kwa alama ya wastani ya 10.467 ikifuatwa na Kapsabet Boys kwa alama ya wastani 10.11.

Mwaka jana, jumla ya watahiniwa 884,263 walifanya mtihani wa KCSE.

Watahiniwa wa kiume walikuwa 405,962 huku wanawake wakiwa 420,845.

View Comments