Wizara ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema Homa ya Nyani MPOX imesababisha vifo vya watu mia tano arobaini na wanane mwaka huu,huku mikoa yote nchini humo ikiripotii visa vya ugonjwa huo.
Waziri wa afya w DRC Samuel Roger Kamba amesema nchi hiyo imerekodi visa takribani 15,600 na zaidi ya vifo mia tano tangu kuanza kwa mwaka huu.
DRC ina majimbo ishirini na sita na idadi jumla ya watu milioni mia moja.
Bwana Kamba amesema Majimbo yaliyoathirika vibaya na MPOX ni Kivu Kusini, Kivu Kaskazini,Tshopo,Equateur,North Ubangi,Tshuapa,Mongala na Sankuru.
Hapo jana,shirika la afya duniani WHO lilitagaza kuwa MPOX ni dharura ya afya ya umma duniani kutokana na kuongezeka kwa visa vya homa hiyo ya nyani DRC na katika mataifa jirani na nchi hiyo.
Uamuzi huo wa WHO ulikuja siku moja baada ya shirika la kudhibiti magonjwa Afrika CDC kutangaza pia MPOX ni dharura ya afya ya umma barani Afrika.