In Summary

•Uchunguzi ulioanzishwa unalenga kubaini ikiwa wanasiasa hao wawili walitenda kosa lolote ili kuchukua hatua.

•Wawili hao ni miongoni mwa wagombea ambao wamekuwa wakimulikwa zaidi kwa madai ya kughushi vyeti vyao vya shahada.

Johnson Sakaja,baada ya kujiwasilisha katika makao makuu ya DCI
Image: RADIO JAMBO

Polisi wameanzisha uchunguzi kubaini uhalisi wa vyeti vya masomo vilivyowasilishwa  kwa IEBC na wagombea ugavana wawili.

Kupitia taarifa yao ya Jumamosi, Tume ya Huduma kwa Polisi (NPS) ilisema wanachunguza vyeti vya mgombea ugavana wa Nairobi kwa tikiti ya UDA Johson Sakaja na Wavinya Ndeti ambaye anawania ugavana wa Machakos kwa tiketi ya Wiper.

Wawili hao ni miongoni mwa wagombea ambao wamekuwa wakimulikwa zaidi kwa madai ya kughushi vyeti vyao vya shahada.

"Kutokana na mamlaka ya kikatiba na kisheria iliyopewa, NPS imeanza uchunguzi wa uhalifu kuhusu uhalisi wa vyeti vilivyowasilishwa kwa IEBC na wawaniaji wawili wa viti vya kisiasa ili waidhinishwe," Taarifa iliyopigwa saini na msemaji wa polisi Bruno Shioso ilisoma.

Aidha Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai ameagiza mkurugenzi wa upelelezi wa jinai kufanya uchunguzi wa haraka kuhusiana na uhalisi wa stakabadhi zote ambazo wagombea ugavana hao wawili waliwasilisha kwa IEBC mapema mwezi huu.

Uchunguzi ulioanzishwa unalenga kubaini ikiwa wanasiasa hao wawili walitenda kosa lolote ili kuchukua hatua.

Sakaja na Wavinya waliidhinishwa na IEBC kugombea ugavana wa kaunti zao mnamo Juni 7 na Juni 11 mtawalia.

Hata hivyo wasiwasi umezuka kuhusu ikiwa watakuwa debeni katika uchaguzi wa mwezi Agosti baada ya malalamishi kuhusu uhalisi wa shahada zao kuwasilishwa mbele ya IEBC ya kutatua mizozo.

Cheti cha Sakaja kutoka chuo kikuu cha Team, nchini Uganda kimetiliwa shaka huku cheti cha Wavinya kutoka chuo kikuu cha South Bank pia kikihojiwa.

Wawili hao hata hivyo wameendelea kusisitiza kuwa vyeti vyao ni halali huku hatima yao ikiwa imebaki kwenye mahakama ya IEBC ya kusuluhisha mizozo.

View Comments