In Summary

•Mechi hiyo ya ufunguzi wa ligi ilichezwa mida ya saa nne usiku wa Ijumaa na Brentford ambayo ilipandishwa ngazi kutoka Championship baada ya kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya tatu ikapata ushindi wa mabao 2-0.

•Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye ni mmoja wa mashabiki sugu wa klabu hiyo ya London ni miongoni mwa walioleza kutoridhika kwao na hali ilivyo pale.

Rais Paul Kagame wa Rwanda
Image: HISANI

Klabu ya Arsenal ilipoteza mechi  yake ya kwanza msimu mpya wa  2021/21 dhidi ya wageni kwenye ligi kuu ya Uingereza,  Brentford.

Mechi hiyo ya ufunguzi wa ligi ilichezwa mida ya saa nne usiku wa Ijumaa na Brentford ambayo ilipandishwa ngazi kutoka Championship baada ya kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya tatu ikapata ushindi wa mabao 2-0.

Bao la kwanza la Brentford lilifungwa  na kiungo wa kati Sergi Canos katika dakika ya 20 huku Christian Norgaard akifunga bao la kufunga mechi katika dakika ya 73.

Matokeo hayo ya kushangaza hayakupokewa vyema na mashabiki wa The Gunners ambao wameendelea kueleza masikitiko yao baada ya kuanza msimu vibaya.

Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye ni mmoja wa mashabiki sugu wa klabu hiyo ya London ni miongoni mwa walioleza kutoridhika kwao na hali ilivyo pale.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kagame amesema kuwa mashabiki wa Arsenal hawafai kuwa wanapitia machungu wanayopata kwa sasa na kudai kuwa  wakati wa mabadiliko umewadia.

"Nini?! Ni soka, Arsenali imepoteza dhidi ya Brentford. Brentford walifaa kushinda na walishinda. Mchezo  wenyewe kando, Arsenal na mashabiki hawafai kuzoea matokeo kama hayo.. HAPANA!! Nasema haya kama mmoja wa mashabiki wakubwa wa Arsenal. Mabadiliko yamechukua muda sana kuja!" Kagame aliandika.

Kulingana na rais Kagame, Arsenal imekabiliwa na hekaheka nyingi ndani ya kipindi cha mwongo mmoja uliopita.

Rais  huyo ambaye ni mmoja wa wafadhili wa klabu hiyo kupitia kampeni ya Visit Rwanda (Tembea Rwanda) amependekeza kuwepo kwa mpango wazi na kumakinika kwa usimamizi wa klabu katika soko la wachezaji.

"Kwani hatuwezi kuwa na mpango ambao unafanya kazi? Kitu kimoja cha kuangalia ni jinsi ya kufanya biashara katika soko ya wachezaji, wachezaji ambao tunanunua ili mpango wetu ufanye kazi. Hatufai kukubali uwastani. Timu lazima ijengwe na nia ya kushinda ndio iwapo tutapoteza hayatakuwa matarajio yetu." Kagame aliendelea kusema.

Kando na Kagame, maelfu ya mashabiki mitandaoni wameendelea kutoa shinikizo la mabadiliko kufanyika katika uongozi wa klabu hiyo ambayo ina historia maalum.

View Comments