In Summary

•Kiungo huyo mkambaji alisema kwamba anajivunia kuwahi wakilisha na kuwa nahodha wa Harambee Stars ila wakati wa kuachia nafasi ile kwa wengine umefika.

•Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amesema kwamba anatazamia kufanya kazi na shirikisho la soka nchini   siku moja ila kwa sasa ataendelea kushabikia Harambee Stars.

Image: TWITTER// VICTOR WANYAMA

Nahodha wa Harambee Stars Victor Mugubi Wanyama alitangaza kustaafu kwake kutoka kwa timu ya taifa siku ya Jumatatu. 

Wanyama ambaye aliwakilisha Harambee Stars kwa mara ya kwanza mwaka wa 2007 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Nigeria alisema kwamba anajivunia kutimiza ndoto yake ya kuwakilisha timu ya taifa.

Kiungo huyo mkambaji alisema kwamba anajivunia kuwahi wakilisha na kuwa nahodha wa Harambee Stars ila wakati wa kuachia nafasi ile kwa wengine umefika.

"Nilipokuwa nakua ilikuwa ndoto yangu kupata nafasi ya kuwakilisha taifa langu. Ninajivunia kusema kwamba nimebahatika kutimiza ndoto yangu.

Kutoka nilipocheza mechi ya kwanza ya kirafiki dhidi ya Nigeria hadi kuwa nahodha wa timu katika mashindano ya AFCON nchini Misri, miaka 14 ambayo imepita imekuwa zaidi ya nilivyotarajia.

Tumekuwa na nyakati nzuri pamoja na ninajivunia kuwahi kuwa nahodha na kiongozi. Lakini kila kitu kizuri huwa na mwisho na hatimaye baada ya kutafakari sana nimefanya uamuzi mgumu wa kustaafu kutoka soka ya kitaifa. 

Wakati umefika niachie wachezaji chipukizi nafasi ili nao pia wasaidie kuendeleza timu ya taifa kufika viwango vya juu" Wanyama alisema.

Isitoshe, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 amesema kwamba anatazamia kufanya kazi na shirikisho la soka nchini   siku moja ila kwa sasa ataendelea kushabikia Harambee Stars.

"Natumai kurejea siku moja nisaidie shirikisho nje ya uwanja lakini hadi wakati huo nitaendelea kuwa shabiki sugu wa Harambee Stars na nitakuwa nawashangilia kutoka nje ya uwanja. Shukran kwa kuniunga mkono" Alisema Wanyama.

Wanyama ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Montreal Impact nchini Canada amewakilisha timu ya Harambee Stars kwa kipindi cha miaka 14 na kushirikishwa kwenye mechi zaidi ya 60.

View Comments