In Summary

•Ruto alisema rais na washirika wake katika kambi ya Azimio la Umoja wameanza mazungumzo yasiyo na maana kwa kutambua kwamba Wakenya wamekataa njama zao za kisiasa.

•Rais alifahamisha takriban wazee 3000 kutoka eneo la Mlima Kenya kwamba Ruto alienda nyuma yake na kujaribu kufikia makubaliano ya mamlaka na kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga ili kumuondoa mamlakani.

Naibu rais William Ruto
Image: MERCY MUMO

Naibu Rais William Ruto amejibu madai ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba alitaka kumtimua mamlakani kabla ya muhula wake kuisha.

Akizungumza katika kaunti ya Kilifi siku ya Jumapili, Naibu Rais alitaja madai ya rais kama propaganda.

Ripoti ya Standard ilisema mzozo kati ya rais na naibu wake ulitimbuka wakati Uhuru aligundua kuwa Ruto alitaka kumng’atua mamlakani.

Lakini Ruto alipuuzilia mbali madai hayo  na kudai kwamba ni uzushi tu.

"Hata kama hamtaki kuniunga mkono, wacheni porojo na propaganda za bure. Wacheni kugawanya wakenya. Eti William Ruto anaweza kupindua mtu ambaye niliweka kwa ofisi?" Ruto alisema.

Gazeti la The Standard lilimnukuu Mbunge wa Mathioya Peter Kimari akisema kwamba rais alifahamisha takriban wazee 3000 kutoka eneo la Mlima Kenya kwamba Ruto alienda nyuma yake na kujaribu kufikia makubaliano ya mamlaka na kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga ili kumuondoa mamlakani.

Gazeti hilo pia lilidai Uhuru alifahamisha wazee kwamba Ruto alikuwa akihimiza maandamano ya upinzani mwaka wa 2017 huku akimchochea Uhuru kuyabana.

Viongozi hao walitoka Kiama Kia Ma, Baraza la Wazee wa Kikuyu na viongozi wengine waliochaguliwa

Lakini siku ya Jumapili, Ruto alisema rais na washirika wake katika kambi ya Azimio la Umoja wameanza mazungumzo yasiyo na maana kwa kutambua kwamba Wakenya wamekataa njama zao za kisiasa.

"Wakenya wamekataa mradi ambao mnataka kutuwekea kimabavu," Ruto alisema

"Mimi ni mtu mzima, mimi si mlevi, mimi si wazimu ati niweke serikali ndani halafu niende niifanyie njama ya kuipindua," Kwa hasira kubwa Ruto alisema.

Akirejelea dhahiri ya Raila, naibu rais alisema kwamba mtu mwenye tabia ya kupindua serikali nchini Kenya anajulikana sana.

"Mnamo 1982, alikuwa huko wakati wa mapinduzi. Hivi majuzi, alijiapisha (kama rais wa wananchi) katika nia ya kujaribu kupindua serikali," Ruto alisema.

"Lazima unanichanganya na mradi wako," Ruto alisema, matamshi ambayo yalionekana kumlenga rais.

"Nataka kusema bila woga wala kinzani. Nataka kuwauliza marafiki zetu, tafadhali, tuwaheshimu sisi tuliompigia kampeni Uhuru Kenyatta na kumfanya rais," Ruto alisema.

Mwezi uliopita, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju pia alidai kuwa Ruto alipanga njama ya kuhujumu utawala wa Uhuru na kuifanya nchi isitawalike.

Madai sawia yalitolewa na naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe mnamo Januari.

Murathe alisema kuwa njama ya Ruto ndiyo sababu kuu ya Uhuru kusalimiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Ruto, hata hivyo, alidai madai hayo ni ishara ya kukata tamaa kutoka kwa kambi ya Azimio ambayo imehisi kushindwa kwa sababu ya kukataliwa kwa mradi wake - Raila Odinga.

“Msilete propaganda zisizo na maana, ukabila hasi kwa sababu hamna mpango na hamna ajenda na kwa sababu mradi wenu umekataliwa na watu wa Kenya,” alisema.

"Kama naibu wa rais, najua ninachopaswa kufanya na sitawahi, sijawahi, na sitawahi na haijawahi kutokea kwamba ningeweza kuwa sehemu ya chochote kitakachoiangusha serikali ya Kenya," DP alisema.

"Wanaoeneza uwongo huo, aibu kwenu! aibu kwenu! hamstahili ila aibu," alihitimisha.

View Comments