In Summary

• Kivutha Kibwana amekashifu uongozi wa vuguvugu la Azimio la Umoja kwa kutoshughulikia maslahi yao.

• Amekanusha madai kwamba vyama vyao ni vidogo, na kwamba wana mchango mkubwa mbele ya uchaguzi mkuu mwezi Agosti.

Gavana wa kaunti ya Makueni ambaye pia ni kinara wa chama cha Muungano, Kivutha Kibwana amezungumza mazito kuhusu madharau wanayoonyeshwa ndani ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance.

Akizungumza na wanahabari, Kibwana alionyesha kughadhabishwa kwake kwa kile alichokitaja kuwa uongozi wa vuguvugu hilo kukosa kuona mchango wao katika mchakato wa kushinda uchaguzi wa Agosti 9.

Kibwana alisema kwamba alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuaminia katika ndoto ya Azimio hata kutupilia mbali azma yake ya urais, hivyo basi anapaswa kupewa heshima anayostahiki.

Alishikilia kwamba maslahi ya vyama vyote kwenye muungano huo lazima yashughulikiwe kwa usawa.

"...Jambo ambalo lipo wazi ni kwamba huwezi kujua chama kikubwa na kidogo kwa sasa, tusubirie baada ya uchaguzi mkuu," Kivutha Kibwana alisema.

Kulingana naye, walitaka manifesto za vyama vyote kushirikishwa kwenye ajenda za muungano huo ili kuhakikisha wahusika wote wanathaminiwa.

Kwa sasa wafuasi wake watalazimika kusubiri kuona iwapo ataendelea kusalia ndani ya Azimio la Umoja One Kenya Alliance ama ataghairi uamuzi huo.


View Comments