In Summary

• John Waluke amesema kwamba ataongoza kampeni za Raila katika eneo la magharibi.

• Alisema kwamba atahakikisha Ruto hashindi kura eneo hilo.

John Waluke
Image: Tony Wafula, KWA HISANI

Mbunge wa eneo la Sirisia, John Waluke amesema kwamba naibu rais William Ruto hawezi kushinda kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu mwezi Agosti.

Waluke alisema kwamba alikuwa amepewa jukumu na rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kuhakikisha kwamba mgombea wa Azimio la Umoja anapata kura nyingi katika eneo la magharibi mwa Kenya.

"...Nipewa hii nafasi, kwa hivyo nawaomba mniunge mkono ili tushinde uchaguzi wa urais," Waluke alisema.

Alisema kwamba lengo lake ni kufanikisha ndoto ya kinara wa ODM kuwa rais wa taifa hili.

Aidha, alisema kwamba Ruto bado ana miaka mingi na anaweza kugombea nafasi hiyo ya urais katika uchaguzi mwingine.

Alisema kwamba wakati huo ukiwadia, kuna uwezekano kwamba atamuunga mkono naibu rais William Ruto kugombea wadhfa wa urais.

Ikumbukwe kwamba John Waluke alikuwa mwanachama wa UDA ila baadaye akaghura akisema kwamba alishawishiwa na rais Uhuru Kenyatta kufanya uamuzi huo.

"Mimi nilikuwa nimelipa ada ya chama huko UDA lakini rais Kenyatta akaniambia nitoke na nisimame na Jubilee," Waluke alisema.

Vilevile alimtaka spika wa seneti Kenneth Lusaka kuwania uongozi wa kitaifa pasi na kujihusisha kwenye siasa za kaunti.

Huku tarehe rasmi ya uchaguzi mkuu ikizidi kukaribia, viongozi mbalimbali wanazidi kubadilisha mirengo yao ya kisiasa ili kuhakikisha kwamba wanajiweka sehemu sawa baada ya shughuli hiyo, huku swali kuu likiwa nani atambwaga mwenzake?

View Comments